Habari Mseto

Mama taabani kukusanya hela za vijana kuwapeleka kazini Afghanistan

August 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE Jumatano alipatwa na mshtuko kundi la vijana zaidi ya 20 waliposimama kortini na kusema amewatapeli maelfu ya pesa akiwandanganya atawapeleka nchini Afghanistan kufanya kazi huko.

Kazi walizokuwa wameahidiwa kufanya ng’ambo ni kufagia , kuosha na kulinda mali.

Walalamishi hao walimweleza hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani, Nairobi Bw Francis Andayi kuwa Bi Ednah Kendi Kiruki amewadanganya kwa miezi mingi.

Wakaeleza dhiki yao, “ Tangu mshtakiwa apokee pesa kwetu imepita miezi mingi na ameshindwa kutupeleka ng’ambo.”

Bw Andayi aliombwa awasaidie walalamishi kulipwa pesa zao .

Lakini Bw Andayi aliwaambia walalamishi kwamba mahakama huamua kesi iliyoshtakiwa.

“Hata mkisimama walalamishi wengi, kama hakuna mashtaka kuwahusu siwezi kufanya chochote,”alisema hakimu.

Aliwashauri walalamishi waende katika kituo cha polisi cha Railways wakae na mshtakiwa waelewane kisha wafike kortini Alhamisi.

Lakini Bi Kiruki alimweleza hakimu kuwa yuko tayari kuwalipa wote pesa alizopokea kutoka kwao katika muda wa wiki mbili