Habari Mseto

Mama wa Taifa azindua teknolojia mpya ya kuchunguza VVU kwa watoto

November 22nd, 2018 2 min read

NA PSCU

MAMA wa Taifa Margaret Kenyatta Alhamisi alijiunga na mwenzake wa Msumbiji, Isaura Nyusi, kuzindua kifaa cha kisasa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga jijini Kisumu.

Bi Kenyatta pia alizindua mpango wa kitaifa wa teknolojia ya utunzi ambapo mamilioni ya watoto wachanga wataweza kunufaika na kifaa hicho kipya cha kuchunguza Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Alisema kifaa hicho kipya kitanufaisha mamilioni ya watoto kote nchini na akaipongeza Wizara ya Afya, Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Maradhi ya Ukimwi pamoja na Maradhi ya kuambukizana kwa kujamiiana (NASCOP) kwa kushirikisha teknolojia hiyo mpya kwenye uchunguzi wa VVU.

Teknolojia hiyo mpya hutoa matokeo papo hapo na hivyo kuwezesha watoto walio katika hatari ya VVU kuanza kutumia dawa za kukabiliana na makali.

Kifaa hicho cha POCEID kinachukua nafasi ya teknolojia ya zamani Polymerase Chain Reaction (PCR) iliyotumika kuchunguza virusi vya Ukimwi kwenye damu. Matokeo ya kifaa hicho huchukua muda wa siku 4 hadi 10.

Kulingana na Afisa Mkuu wa hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga Dkt Peter Okoth, wakati mwingine kifaa hicho hutoa matokea yasiyo na ukweli ya watoto wanaozaliwa baada ya kutambua antijeni za mama.

Uchunguzi wa VVU miongoni mwa watoto kwa kutumia teknolojia ya PCR hufanyika katika maabara ya taasisi ya utafiti wa matibabu nchini, KEMRI kituo cha Kisian, yapata kilomita 15 kutoka hospitali ya mafunzo na rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga.

Katika hospitali hiyo, Mama wa Taifa na mwenzake wa Msumbiji walipokelewa na kuonyeshwa katika taasisi hiyo na Gavana wa Kaunti ya Kisumu Prof. Anyang Nyong’o, Afisa Mkuu Dkt. Peter Okoth, Waziri wa Afya kwenye Kaunti Dkt. Rosemary Obara, Katibu wa Kaunti Dkt. Olango Onudi na Mkurugenzi wa Afya Dkt. Dickens Onyango.

Miongoni mwa wagonjwa waliotembelewa na Mama hao wa Mataifa ni wanawake 60 wanaoendelea kupona kutokana na upasuaji baada ya kuugua nasuri, yani fistula.

“Nilitembelea zaidi ya wanawake 60 ambao wameathirika kutokana na fistula. Leo wamepewa matumaini, hawatateseka kutokana na unyanyapaa na fedheha. Ni akina mama, wanawake na dada zetu na naomba kwamba tuwakumbatie na kushirikisha wanawake hawa ili wao pia wachangie ustawi wa jamii zao,” akasema Mama wa Taifa.