Shangazi Akujibu

Mamake demu wangu amenipa ombi la kushangaza

April 19th, 2024 1 min read

Shangazi,

Mpenzi wangu ndiye mtoto wa pekee na mama yake hajaolewa. Juzi nilishangaa mama yake aliponipigia simu akisema ananipenda na kuniomba niachane na binti yake ili tuwe wapenzi. Nifanyeje?

Ni makosa kwa mama kunyemelea mpenzi wa binti yake. Lakini si hatia kwa sababu yeye pia ni binadamu na anatamani kupenda na kupendwa. Amekuomba tu, si lazima. Sasa utaamua kati yake na binti yake.

Jamaa wa mke wangu wamenigeuza benki

Hujambo Shangazi. Nimeoa lakini sina amani katika ndoa kwa sababu ya watu wa familia ya mke wangu. Wamezoea kunipa mahitaji yao ya pesa na wakati mwingine nalazimika kunyima familia yangu ili niwape. Nifanye nini?

Tabia ya jamaa za wakwe zako inaweza kuzua ugomvi kati yako na mke wako hasa ukiendelea kunyima familia kwa sababu yao. Mwelezee unavyohisi kisha umtume azungumze nao.

Nilitarajia aseme pole kwa kosa lake

Nilimuacha mpenzi wangu miezi mitatu iliyopita baada ya kunikosea. Nilidhani ataniomba msamaha ili turudiane lakini amenyamaza tu. Nitakosea kutafuta mwingine?

Hatua ya mpenzi wako kukatiza kabisa mawasilino ni ishara kwamba ameamua huo ndio mwisho wa uhusiano wenu. Usiendelee kufunga moyo wako kwa ajili ya mtu asiye na haja nawe. Tafuta mapenzi.

Heri nibakie singo kuliko kusalitiwa na mpenzi

Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28 na sijawahi kuwa na mpenzi. Natamani sana kuwa naye lakini naogopa wanaume. Naomba ushauri.

Usiwe na wasiwasi. Kila mtu ameumbwa tofauti na wengine. Baadhi ya maumbile hubadilika jinsi mtu anavyokua. Hatimaye woga wa kujumuika na kuzungumza na wanaume utakutoka.