Bambika

Mamake Diamond amfosi kuoa

March 13th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO

MPANGO wa mamake Diamond kumwoza mke mwanawe huyo staa wa muziki umetibuka.

Esna Khan, dadake staa wa Bongo Flava Diamond Platnumz, amefichua tukio la jinsi mama yao, Sandra, alivyomfosi nyota huyo kuoa.

Esma amekiri kuwa suala la kutaka kumwona kaka yake akifunga ndoa limekuwa ndio matamanio ya familia yao kwa siku nyingi sana.

Hata hivyo chelewa chelewa ya mdogo wake anayejulikana kuwa sukari ya warembo imeendelea kuwaumiza sana.

Akifunguka za ndani kuhusu mchakato ambao familia imekuwa ikiendesha kumshurutisha Diamond kuoa, Esma anakiri kwamba kuna kipindi nusura presha yao izae matunda.

“Suala la kuoa huyo tushaongea naye sana. Tulijaribu kumfosi aoe lakini tukamwona muda wake mwenyewe ulikuwa bado,” kafichua Esma.

Na je jitihada zao zilifikia wapi?

“Kulikuwa kuna mwanamke mmoja anaitwa Sofia. Alipelekewa mpaka mahari, ikawa imebaki siku sisi kuenda kujitambulisha ukweni rasmi kwenye uchumba. Na yeye mwenyewe Diamond na wapambe wake walikuwa wameshashona nguo za sare kutoka Uturuki. Kila kitu kilikuwa kimeandaliwa mpaka hata mwanamke alikuwa ameshafika hapa kwetu. Na yeye Diamond alikuwa na amsha amsha kweli lakini siku zilipokaribia akaona hayuko tayari. Alimfuata yule mwanamke na kumwambia amekaa amefikiria na kuona hayuko tayari,” akafichua.

Kulingana na Esma, hatua hiyo ilimuumiza sana mama yao kiasi cha kumtishia Diamond na laana.

“Mama alimfosi mpaka ilifikia kipindi akawa anamwambia ‘kama kweli mimi ni mamako wajua…’ Kauli ya mama yetu Sandra ilikuwa ile ya mtu kumtishia mtu. Lakini alikaa na mamake akamwambia ‘hivi nikimchukua mtoto wa watu, nimwingize ndani halafu nikamtesa, huoni kama nitakuwa naidhulumu nafsi yake? Muda wangu ukifika nitaoa’. Kwa hiyo sisi tulimwelewa,” akasema Esma.