Habari

Mamake Mevis sasa amtenganisha na pacha Melon na Sharon

June 21st, 2019 1 min read

Na BENSON AMADALA

MAMAKE msichana aliyelelewa pamoja na mmoja wa pacha wa Kakamega ambao taarifa zao zimekuwa zikipata umaarufu, Ijumaa asubuhi amemchukua mwanawe na kuibua hali ya kutoelewana baina ya familia mbili.

Kumeshuhudiwa hali ya mshikemshike Bi Angelina Omina, akiandamana na maafisa wa polisi, alimchukua binti yake, Mevis Imbaya, wakati ambapo jamaa za pacha wawili walikuwa wakijiandaa kukutana na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.

Jamaa hao walikuwa na wasichana hao pacha pamoja na Mevis.

Bi Omina amewalaumu jamaa hao kwa kumshinikiza binti yake kuendelea kuishi na Bi Rosemary Onyango, mamake pacha hao nyumbani kwake Fufural, Kaunti ndogo ya Likuyani.

Kwenye patashika hiyo, jamaa wa pacha hao, Shem Abuti, amehangaishwa kwa kujaribu kuwazuia maafisa kumchukua Mevis na kumkabidhi kwa mamake.

“Wasichana hawa walikuwa wamefanya uamuzi bila kushinikizwa kwamba wataendelea kuishi pamoja baada ya ripoti ya uchunguzi wa vinasaba (DNA), lakini sasa tunaona hujuma katika hili,” amesema Bw Abuti.

Sharon Matius, Mevis Imbaya na Melon Lutenyo, wakiwa kijini Furfural, Kaunti ya Kakamega Aprili 16, 2019. Picha/ Maktaba