Habari

Mambo bado kwa gavana Obado na wanawe wanne

August 27th, 2020 2 min read

Na RUTH MBULA

GAVANA wa Migori Okoth Obado na wanawe wanne Jumatano walijisalimisha kwa afisi za Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) mjini Kisii kufuatia agizo la Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) mnamo Jumanne kwamba wakamatwe.

Bw Obado alihojiwa kwa saa tatu na maafisa wa tume hiyo ambapo baadaye alisafirishwa hadi jijini Nairobi.

Gavana anadaiwa kuipora kaunti hiyo zaidi ya Sh70 milioni kwa kushirikiana na wanawe.

Mnamo Jumanne, DPP Noordin Haji aliagiza washukiwa hao wakamatwe, baada ya uchunguzi kubaini kuna ushahidi wa kutosha walishiriki kwenye uporaji huo.

“Kila kitu ki’ shwari,” akasema Bw Obado kwa wanahabari ambao walikuwa wamepiga kambi nje ya afisi hizo.

Wanawe pia hawakuonyesha hali yoyote ya wasiwasi ambapo kama baba yao, walisafirishwa jijini Nairobi pia. Wanne hao ni Susan Scarlet, Jerry Zachary, Evelyn Adhiambo na Dan Achola Okoth.

Bw Obado ambaye anahudumu kwa muhula wa pili, alifika kwenye afisi hizo mwendo wa saa mbili unusu asubuhi, akiwa ameandamana na jamaa zake, wasaidizi na baadhi ya wafanyakazi wa kaunti.

Wanahabari, wafuasi wake na marafiki walizuiwa kuingia ndani.

Kwa mujibu wa DPP, gavana alipokea Sh73.4 milioni kutoka kwa kampuni ambazo zilifanya biashara na serikali ya kaunti alipohudumu muhula wa kwanza.

Duru katika tume hiyo zilisema kwamba, washukiwa 10 kati ya 11 ambao walijisalimisha ili kuhojiwa, walikamatwa na kusafirishwa jijini Nairobi.

Kwenye agizo lake, Bw Haji alisema wanawe Obado walipokea Sh34.5 milioni kutoka kwa kampuni zinazohusishwa na nduguye watatu gavana. Alisema walikuwa mawakala wa baadhi ya kampuni zilizotajwa.

“Fedha za umma zilipotea kupitia njama ambapo gavana alishirikiana kisiri na baadhi ya kampuni zilizopokea malipo kutoka kwa serikali ya kaunti. Zilitoa hongo ili kupewa kandarasi,” akasema Bw Haji.

Uchunguzi wa EACC unaonyesha kuwa, kampuni hizo tatu zilituma Sh38.9 milioni kwa wanawe Bw Obado. Fedha hizo zinadaiwa kuwalipia karo za shule, matumizi ya kibinafsi na gharama za matibabu. Watatu hao walikuwa wakisomea katika nchi za Australia, Scotland na Uingereza.

Uchunguzi pia ulibaini kwamba, Sh34.5 milioni zilitumika kununua nyumba katika mtaa wa kifahari wla Loresho, Nairobi, inayomilikiwa na mwanawe, Evelyn Adhiambo.