HabariSiasa

MAMBO NI MAGUMU

October 4th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MALUMBANO kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, yamemwongezea Rais Uhuru Kenyatta matatizo yanayomkabili anapopambana na matatizo chungu nzima wanayopitia Wakenya.

Japo muafaka wake na Bw Odinga ulilenga kuweka mazingira ya kufanikisha Ajenda Nne Kuu za Maendeleo na kupigana na ufisadi, kwa sasa yuko katika hali ya mshikemshike kuhusu mwelekeo anaofaa kuchukua kwenye vita kati ya naibu wake na Bw Odinga.

Hii ni ikizingatiwa kuwa wawili hao ni muhimu katika utawala wake na hivyo kushindwa kwao kufanya kazi pamoja kunatishia mafanikio ya utawala wake.

Bw Ruto ni muhimu kwa Rais Kenyatta kwani ndiye naibu wake, na mchango wake katika kuhakikisha utulivu serikalini. Pia anamhitaji Bw Ruto kuhakikisha Jubilee hakivunjiki na pia utulivu unadumishwa hasa katika ngome yake ya kisiasa ya Rift Valley.

Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta anamhitaji Bw Odinga kutokana na ufuasi alio nao kitaifa, na uwezo wake kutatiza shughuli za serikali iwapo watakosana. Hii inadhihirika na utulivu unaoshuhudiwa kote nchini tangu walipoafikiana kushirikiana. Pia anahitaji uungwaji mkono wa Bw Odinga katika vita dhidi ya ufisadi na kutimiza ahadi ya kuwaunganisha Wakenya.

Katika hali hii, Rais Kenyatta anajipata katika njia panda, kwani uamuzi wowote ule utakuwa na madhara kwa utawala wake.

Wadadisi wanasema chaguo lake sasa ni kujaribu kutumia mbinu za kidiplomasia kuhakikisha Bw Ruto na Bw Odinga wanakomesha vita vyao na kufanya kazi naye kwa pamoja. Lakini si jambo lahisi kupatanisha wawili hao ikizingatiwa kila mmoja ana azma ya kumrithi Rais Kenyatta, na hivyo kila hatua wanayopiga inalenga uchaguzi wa 2022.

Bw Ruto anadai Bw Odinga alitumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kujiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma, naye Raila anadai kwamba Ruto anahofia juhudi zake na Rais za kupigana na ufisadi.

Mvutano wa wawili hao umeleta mgawanyiko katika chama tawala cha Jubilee huku wafuasi wa Rais na wale wa Bw Ruto wakitofautiana kuhusu wajibu wa Bw Odinga serikalini.

Wale wa Bw Ruto wanadai kuwa Bw Odinga anataka kumwekea vizingiti Naibu Rais katika safari yake ya kuingia Ikulu 2022 kama alivyokubaliana na Rais wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana, nao wale wa Rais wanadai hawana deni la kisiasa la kumlipa Naibu Rais.

Katika kambi ya Bw Ruto ndani ya Jubilee kuna hisia kuwa Rais amemkumbatia zaidi Bw Odinga kuliko naibu wake.

Mzozo wa Bw Ruto na Bw Odinga unamwongezea Rais Kenyatta matatizo likiwemo la mwito wa marekebisho ya Katiba, ambapo Bw Odinga na wafuasi wake wakiwemo baadhi ndani ya Jubilee wanaunga mkono, huku wale wa Bw Ruto wakipinga.

Rais Kenyatta pia amejipata kwenye hali ngumu ya siasa za watu wawili anaohitaji sana wakati anapojikuna kichwa kuhusu deni la Sh5 trilioni linalodaiwa Kenya.

Rais alikopa madeni hayo kufadhili miradi ya maendeleo, lakini amejipata katika hali ambapo uchumi hauna uwezo wa kuyalipa. Hili limemwacha katika njia panda kuhusu atakakotoa pesa za kulipa madeni hayo na wakati huo huo kutekeleza miradi ya ustawi wa nchi.

Hili limemlazimu kuwasukumia wananchi mzigo mzito wa ushuru. Madeni hayo na kupanda kwa gharama ya maisha kumefanya umaarufu Rais Kenyatta na serikali yake kushuka pakubwa hata katika ngome zake za kisiasa.

Tatizo lingine linalomkumba Rais Kenyatta ni kuwa wabunge wa chama chake anaotengemea kufanikisha ajenda za serikali hasa kwa kutunga sheria zinazohitajika, wameanza kuonyesha uasi kwake kama ilivyoshuhudiwa kwenye kikao maalum cha kujadili mapendekezo yake ya ushuru mwezi Oktoba.