Michezo

Mambo ni unyo unyo ‘Ndovu’ Arsenal ikikanyaga Luton na kurejea juu ya mti

April 4th, 2024 2 min read

LONDON, Uingereza

KOCHA Mikel Arteta amejaa furaha baada ya vijana wake kubwaga Luton Town 2-0 licha ya kuwa hakuna nafasi ya kupumua, huku Arsenal, Liverpool na Manchester City wakifuatana unyo kwa unyo katika nafasi tatu za kwanza.

Wanabunduki wa Arsenal walikung’uta Luton kupitia mabao ya Martin Odegaard dakika ya 24 na Daiki Hashioka aliyejifunga dakika ya 44 ugani Emirates na kurukia kileleni kwa alama 68. Emile Smith Rowe aliibuka mchezaji bora kuchangia katika kuzalishwa kwa magoli yote mawili.

“Tunaonyesha uimara na ubora kuendelea kupigania taji. Macho sasa tunatupia mchuano ujao dhidi ya Brighton,” akasema Arteta.

Mabao hayo yalisaidia Arsenal kuandikisha historia ya kuwa klabu ya kwanza kabisa kufunga jumla ya mabao 25 dhidi ya timu zilizopanda ngazi katika msimu mmoja. Washiriki wapya msimu huu ni Luton, Burnley na Sheffield United ambao wamekula mabao 6-3, 8-1 na 11-0 kutoka kwa Arsenal, mtawalia.

Hata hivyo, vijana wa kocha Mikel Arteta wanatarajiwa kung’olewa kileleni na Liverpool ikiwa vijana wa kocha Jurgen Klopp watapepeta wavuta-mkia Sheffield United ugani Anfield Alhamisi usiku inavyotarajiwa. Reds wanaingia uwanjani wakiwa na alama 67 na mchuano mmoja mkononi.

Mabingwa watetezi City, ambao walipumzisha nyota Kevin De Bruyne na Erling Haaland, wana pointi 67 baada ya kushinda mechi yao ya 30 kwa kuchabanga Aston Villa 4-1 kupitia mabao ya Phil Foden (matatu) na Rodri.

Vijana wa kocha Pep Guardiola sasa hawajapoteza mechi 40 nyumbani katika mashindano yote ikiwa ni mara yao ya pili kufanya hivyo tangu Desemba 1919 hadi Novemba 1921.

Villa, ambao kichapo hicho kilikuwa chao cha kwanza ugenini ligini mwaka huu, walipata bao la kufutia machozi kutoka kwa Jhon Duran.

Vijana wa kocha Unai Emery wana alama 59. Wako katika vita vikali na Tottenham vya kuingia Klabu Bingwa Ulaya moja kwa moja ikiwa nambari tano Tottenham watazima Nottingham Forest (17) hapo Aprili 7.

Katika mechi nyingine Jumatano, wenyeji Brentford walibahatika kuponyoka na alama moja katika sare tasa dhidi ya Brighton iliyomiliki mchezo huo kwa makombora 24-5, makombora yaliyolenga lango 6-2, umilikaji wa mpira 68-32, pasi 663-326 na kona 5-1.

Brighton iliyotangaza kupata faida ya Sh20.2 bilioni msimu 2022-2023 mnamo Jumatatu, inakamata nafasi ya tisa kwa alama 43 nayo Brentford iko katika nafasi ya 15.