Mamelodi Sundowns yatinga 16-bora Nedbank Cup bila Mkenya Brian Mandela

Mamelodi Sundowns yatinga 16-bora Nedbank Cup bila Mkenya Brian Mandela

Na GEOFFREY ANENE

Beki Mkenya Brian Mandela Onyango alikuwa shabiki tu timu yake ya Mamelodi Sundowns ikitupa Stellenbosch FC nje ya Kombe la Nedbank baada ya ushindi wa mabao 3-2 uwanjani Loftus Versfeld mnamo Jumatano.

Onyango alikuwa katika orodha ya wachezaji watano ambao Sundowns ilikosa katika mchuano huo. Nyota huyo wa Harambee Stars yuko mkekani akiuguza jeraha la paja alilopata dhidi ya SuperSport kwenye Ligi Kuu mnamo Januari 16. Amekosa mechi tano sasa.

Wageni Stellenbosch walitangulia kutikisa nyavu za mabingwa hao wa Afrika Kusini dakika ya 12 kupitia Ashley Du Preez aliyemwaga kipa mpya Ricardo Goss.

‘The Brazilians’ wanavyofahamika Sundowns kwa jina la utani, walisawazisha 1-1 kupitia Mnamibia Peter Shalulile dakika nne baadaye baada ya kuwazidia kasi mabeki na kisha kuachilia shuti tamu wavuni. Hakuna aliyeona lango la mwingine tena katika kipindi cha kwanza.

Mabao zaidi yalipatikana dakika za lala-salama. Mabadiliko mawili kwa mpigo dakika ya 86 kwa upande wa Sundowns yalishuhudia timu hiyo ikichukua uongozi dakika ya kwanza ya majeruhi kupitia raia wa Uruguay Gaston Sirino. Hata hivyo, Nange alifanya mabao kuwa 2-2 dakika ya tatu ya majeruhi.

Shalulile alihakikishia Sundowns ushindi alipofunga bao la tatu dakika ya 117 baada ya refa kuongeza dakika 30. Ushindi huo uliweka Sundowns katika mduara wa 16-bora wa kipute hicho.

You can share this post!

Festus Mwoki ashinda mbio za nyika za Pwani

Wazazi wa wanafunzi wanaoteketeza mabweni walipe gharama...