NA SIMON CIURI
MAHAKAMA ya Kiambu Jumatano iliwakubalia polisi kuwazuilia mameneja tisa wa kampuni ya kusambaza stima ya Kenya Power kwa siku nane ili kuwapa muda wa kukamilisha uchunguzi kuhusu madai kuwa walihusika katika kuvuruga huduma za stima kote nchini wiki iliyopita.
Mameneja hao ni David Kamau, George Kipkoech, Jukius Karani, Geoffrey Kipkirui, Anthony Gathii, Martin Musyoki, Joshua Wasakha, Raphael Ndolo na Peter Musyoki
Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kahawa, Boaz Ombewa alisema warudishwe kortini Januari 26.
Kulingana na upande wa mashtaka, kupotea kwa stima siku hiyo katika maeneo mengi ya nchi kulifanywa kimakusudi kutokana na wahusika kuzembea kazini.
Afisa anayechunguza kesi hiyo, Bw Keith Robert alisema kulikuwa na hatari ya tisa hao kuhujumu uchunguzi wa polisi iwapo wangeachiliwa kwa dhamana.
Mawakili wa washtakiwa walipinga kesi hiyo wakisema wateja wao wanaonewa.