Kimataifa

Mamilioni watoroka makazi yao wakihofia kudhulumiwa kimapenzi

March 29th, 2018 1 min read

Na AFP

VISA vya dhuluma za kimapenzi vimeongezeka eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hali hiyo imesababisha mgogoro wa kibinadamu na kulazimisha mamilioni kutoroka makwao.

Takriban raia 13.1 milioni wa Congo wanahitaji misaada ya chakula, nguo na malazi ambao ni pamoja na 7.7 milioni wasio na chakula kabisa.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wiki iliyopita, katika taarifa ya pamoja.

Lakini serikali ya Congo imepuzilia mbali taarifa hiyo ikisema imeongezwa chumvi. Huku majibizano hayo yakiendelea, visa vya ubakaji na unajisi vimeongezeka katika eneo hilo linaloendelea kukumbwa na vita.

DR Congo wiki iliyopita ilijiepusha na mkutano mkubwa wa mashirika ya utoaji wa misaada ya kibinadamu, Geneva, unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

“Mnamo 2015, visa vya dhuluma za kimapenzi vilipungua kwa kiasi kidogo,” alisema daktari wa kina mama Denis Mukwege, ambaye kwa mara tatu ameteuliwa kwa Tuzo la Amani la Nobel kutokana na kazi yake ya kuwasaidia waathiriwa wa ubakaji na unajisi eneo hilo.

“Tangu mwishoni mwa 2016 na 2017, kumekuwa na ongezeko la visa vya dhuluma za kimapenzi,” aliambia AFP hospitalini mwake, jijini Bukavu, ambako huwatibu wanawake waliobakwa au wasichana walionajisiwa.

Mmoja wa manusura, msichana wa miaka 10 alinajisiwa na wapiganaji Februari, walipovamia kwao kijijini Kabikokole.

Mukwege alisema aina ya wabakaji na wanajisi imebadilika. “Visa vingi sasa vinatekelezwa na watu wa kawaida eneo la Kivu Kusini. Sio tena wanajeshi au wapiganaji,” alisema.

Hata hivyo, watu wengi eneo hilo walikuwa wapiganaji, ulisema wakfu wa Panzi. Wakati huo, migogoro kati ya makundi tofauti ya wapiganaji, waasi, makundi ya vijana ya kudumisha amani, na jeshi la Congo kusababisha vifo zaidi.

Kulingana na kundi la utafiti Congo Research Group, wanajeshi pekee walisababisha vifo 106 na waliteka nyara watu 80 eneo la Kivu Kaskazini Februari.

Katika mji wa Goma, Kivu Kaskazini, Hospitali ya Bethesda, inayoendeshwa na Shirika la Msalaba Mwekundu uhudumia watu waliopigwa risasi.