Mamilioni ya fedha Henry Meja atazoa baada ya kujiunga na AIK

Mamilioni ya fedha Henry Meja atazoa baada ya kujiunga na AIK

Na GEOFFREY ANENE

Mshambuliaji Henry Atola Meja yuko mbioni kuingia kundi la mamilionea baada ya kazi yake safi uwanjani kushuhudia klabu ya AIK nchini Uswidi ikimnyakua kwa kandarasi ya miaka mitano itakayokatika Septemba 1, 2026.

Tusker inaaminika inalipa wachezaji wake kati Sh360,000 na Sh960,000 kila mwaka mbali na marupurupu ya Sh10,000 kwa kuandikisha ushindi na Sh5,000 kwa kupiga sare. Mshahara wastani wa mchezaji kwenye Ligi Kuu ya Uswidi ni Sh14,519,916 kwa mwaka (Sh1,209,993 kila mwezi).

AIK, ambayo imeajiri beki Mkenya Eric “Marcelo” Otieno, inashiriki ligi hiyo maarufu kama Allsvenskan. Imekalia juu ya jedwali la msimu huu wa 2021 kwa alama 36, mbili mbele ya Djurgarden nao mabingwa watetezi Malmo wako katika nafasi ya tatu kwa alama 33 baada ya mechi 17.

Meja atafikisha umri wake kuwa miaka 20 mnamo Desemba 21 mwaka huu.

“AIK Fotball imefikia makubaliano na Tusker FC kuhusu uhamisho wa mchezaji mwenye umri wa miaka 19 wa timu ya taifa ya Kenya Henry Atola Meja. Makubaliano hayo yako hai hadi Septemba 1, 2026,” ilitangaza klabu hiyo iliyoshinda Allsvenskan mara ya mwisho mwaka 2018.

AIK iliongeza, “Mchezaji huyu atajiunga na timu yake mpya mara tu stakabadhi yake ya kazi itakuwa tayari, lakini hataweza kutuchezea hadi Januari 2022 soko la uhamisho la Uswidi litakapofunguliwa.”

Mzawa huyo wa kaunti ya Kakamega na mchezaji wa zamani wa klabu ya Lirembe Arsenal alifurahia fursa ya kuwa atachezea AIK.

Mkurugenzi wa michezo wa AIK, Henrik Jurelius alimsifu Meja kama mchezaji aliye na talanta kubwa ambaye wanatumai “ataimarika zaidi chini ya uangalizi wetu”.

Msimu uliopita, Meja alifunga mabao 11 yakiwemo manne yaliyomfanya iabuke mchezaji bora Ligi Kuu ya Kenya wa mwezi wa Januari 2021.

Mara ya kwanza Meja ailijumuishwa katika timu ya taifa ilikuwa Februari 2021. Kocha Jacob “Ghost” Mulee alimtumia kwenye mechi kwa mara ya kwanza katika mechi ya kirafiki dhidi ya Tanzania mnamo Machi 15 ambayo Harambee Stars ilishinda 2-1 ugani Nyayo. Aliingizwa katika mechi hiyo katika nafasi ya Lawrence Juma dakika ya 70.

Yuko katika kikosi cha Stars kilicho jijini Kigali kuvaana na wenyeji Rwanda katika mechi ya pili ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 itakayosakatwa Septemba 5.

Meja alikuwa kitini katika sare ya 0-0 dhidi ya Uganda Cranes katika mechi ya kwanza ya Kenya kwenye Kundi E.

Ametiwa katika orodha ya wawanizi wa tuzo ya chipukizi bora kwenye Ligi Kuu ya Kenya msimu 2020-2021. Anawania tuzo hiyo dhidi ya Lewis Bandi (AFC Leopards), Lawrence Luvanda (Vihiga United), Frank Odhiambo (Gor Mahia), Sylvester Owino (Kakamega Homeboyz), Rodgers Ouma (Western Stima) na Ambrose Sifuna (Sofapaka). Mshindi wa tuzo hiyo atajulikana Septemba 11.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wakataa pendekezo la kupunguza riba ya mikopo ya...

Omanyala azoa laki mbili akimaliza nambari nne Riadha za...