Mamilioni ya Ruto yawasha moto sehemu tofauti nchini

Mamilioni ya Ruto yawasha moto sehemu tofauti nchini

GITONGA MARETE na DAVID MUCHUI

MAMILIONI ya fedha ambazo Naibu wa Rais William Ruto amekuwa akimwaga kila mahali anapozuru, yanazidi kupiganisha ‘mahasla’ kote nchini.

Ziara ya Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya imesababisha mivutano katika maeneo mbalimbali ambapo wafuasi wake wanapigania fedha hizo za bwerere.

Wahudumu wa bodaboda katika eneobunge la Tigania Mashariki, Ijumaa waliandamana wakitaka kupewa Sh600,000 walizodai zilitoka kwa Dkt Ruto alipozuru eneo hilo, Jumanne.

Wahudumu hao walitatiza shughuli za usafiri kwa muda walipochoma magurudumu barabarani wakidai mgao wao.

Dkt Ruto alipozuru eneo hilo alitangaza kutoa Sh300,000 kwa wahudumu wa bodaboda na Sh300,000 kwa makundi ya wanawake.

Dkt Ruto alikuwa ameandamana na mbunge wa Tigania Magharibi, Dkt John Mutunga, ambaye alieleza umati wa watu waliofika kuwalaki kwamba, mwenzake wa Tigania Mashariki, Bw Gichunge Kabeabea, alikuwa ziarani nje ya nchi.

Waandamani hao jana walishutumu Bw Kabeabea ambaye walidai kuwa aliagiza fedha walizopewa na Dkt Ruto zihifadhiwe hadi atakaporejea nchini kutoka ughaibuni.

“Tumeelezwa kuwa pesa hizo haziwezi kutolewa hadi mbunge wetu atakaporejea. Mbunge hahusiki kwa vyovyote na pesa hizo na tunataka Naibu Rais aamrishe zitolewe mara moja,” alisema Bw Jackson Muriki, mhudumu wa bodaboda.

Wahudumu hao waliozua fujo walifunga barabara ya Meru-Maua – hali iliyolazimu maafisa wa polisi kuwatawanya kwa vitoa machozi.

Naibu Rais alikamilisha Ijumaa kampeni zake katika Kaunti ya Embu na kusisitiza kwamba chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kitashinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Aliwataka wakazi wa eneo la Mlima Kenya kumkataa kinara wa ODM Raila Odinga huku akidai kwamba amezeeka na ameishiwa na nguvu za kuongoza nchi.

Katika eneo la Igembe Kaskazini, wanasiasa wawili wanaomezea mate viti mbambali vya kisiasa mwaka 2022, walizozana hadharani kuhusiana na Sh300,000 zilizodaiwa kutolewa na Dkt Ruto.

You can share this post!

Njaa ilivyouza magaidi

DOUGLAS MUTUA: Kuwaadhibu wakuu wa magereza ni...

T L