Mamilioni ya Wakenya washiriki uchaguzi leo

Mamilioni ya Wakenya washiriki uchaguzi leo

NA LEONARD ONYANGO

WAKENYA leo Jumanne wanachagua viongozi 1,882 watakaoshikilia nyadhifa mbalimbali za kisiasa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Vituo vya kupigia kura vinafunguliwa saa 12.00 asubuhi na kufungwa saa 11.00 jioni.

Kulingana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), watu 22,120,458 wamesajiliwa kuwa wapigakura na wagombea 16,098 wanawania viti mbalimbali kuanzia urais, ugavana, useneta, ubunge, uwakilishi wa wanawake na udiwani.

Wapigakura watachagua mmoja kati ya Naibu wa Rais William Ruto wa United Democratic Alliance (UDA), Bw Raila Odinga (Azimio la Umoja), Prof George Wajackoyah (Roots) na Bw Mwaure Waihiga (Agano) kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta anayestaafu.

Baada ya kuonyesha kitambulisho cha kitaifa au paspoti na kutambuliwa kwa kutumia kifaa cha kielektroniki cha kutambua wapigakura (Kiems) kituoni, mpigakura atapewa karatasi sita za rangi tofauti kulingana na kiti.

Kila karatasi ni sharti iwe imepigwa muhuri wa IEBC nyuma ili iweze kuhesabiwa kuwa kura halali.

Wapigakura wakiwa kwenye foleni katika Shule ya Msingi ya Kahuho. PICHA | SAMMY WAWERU

Karatasi isiyo na muhuri inachukuliwa kuwa imeharibika.

Baadaye, mpigakura ataenda kwenye kibanda cha kupigia kura na kuchagua viongozi anaowataka.

Baada ya kutia alama, mpigakura anatumbukiza karatasi ‘debeni’ kulingana na wadhifa.

Karatasi ya kura inayopatikana katika debe lisilofaa inachukuliwa kuwa imeharibika.

Kwa mfano, karatasi ya kura ya urais ikipatikana ndani ya debe la wawaniaji wa udiwani wakati wa kuhesabu, inachukuliwa kwamba imeharibika.

Kabla ya kuondoka kituoni, mpigakura anawekewa wino kama ishara ya kuonyesha kwamba tayari amepiga kura.

Katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017, jumla ya kura 403,503 zilikataliwa baada ya kupatikana na dosari mbalimbali.

Kura huchukuliwa kuwa imeharibika iwapo mpigakura ataweka alama kwenye visanduku vya zaidi ya mgombea mmoja.

Mpigakura asipoweka alama yoyote pia kura inaharibika.

Baada ya kura kuhesabiwa, maajenti watahitajika kuweka saini kabla ya nakala kutumwa katika Kituo cha Kitaifa cha Kujumulisha Matokeo katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Nakala za matokeo zinatumwa kwa kutumia kifaa cha Kiems.

Jumla ya vifaa vya Kiems 55,100 vimetawanywa katika vituo vya kupigia kura 46,229 kote nchini, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati.

“Kila wadi imepewa vifaa sita vya Kiems vya ziada kwa tayari kutumika iwapo kutakuwa na hitilafu,” alisema Bw Chebukati.

Jumla ya watu 2,132, wakiwemo wanawake 225, wanawania ubunge. Wawaniaji 341 – wakiwemo wanawake 43 – wanagombea useneta na 266 wanawania ugavana.

Kiti cha udiwani ndicho kimevutia idadi kubwa ya wawaniaji kwani wagombea 12,994 wamejitosa ulingoni kung’ang’ania viti 1,450.

Wakazi wa eneobunge la Mugirango Kaskazini, Kaunti ya Kisii, watakuwa na kibarua kigumu cha kuchagua mbunge wao kwani karatasi ina wawaniaji 17, akiwemo mbunge wa sasa Joash Nyamoko anayetetea kiti chake kupitia tiketi ya UDA.

Wakazi wa Kaunti ya Taita Taveta watakuwa na karatasi ndefu zaidi ya ugavana kwani wawaniaji 12 wamejitokeza kupambana na gavana wa sasa Granton Samboja.

Wakazi wa Kaunti ya Vihiga ndio watakuwa na karatasi ndefu zaidi ya useneta kwani watu 14 wamejitokeza kumrithi Seneta George Khaniri anayewania ugavana.

Huku wawaniaji 16,098 wakishikilia roho mkononi kutokana na hofu ya kubwagwa, wawaniaji watatu tayari wametangazwa washindi na IEBC baada ya kukosa wapinzani.

Wanaongojea kuapishwa ni Bi Beatrice Kemei, mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kericho, kupitia tiketi ya UDA.

Wengine ni madiwani wateule Julius Kimutai (Ravine, Baringo) na Issa Aden (Sabena, Garissa).

  • Tags

You can share this post!

Viongozi waelezea matumaini ya uchaguzi wa amani

Makamishna na wakuu wenye kibarua uchaguzi ukifanyika

T L