Mamilioni yapotelea kwenye miradi duni

Mamilioni yapotelea kwenye miradi duni

Na MAUREEN ONGALA

MIRADI ya kunyunyiza maji mashambani iliyoanzishwa katika Kaunti ya Kilifi imeshindwa kuletea maelfu ya wakazi eneo hilo afueni, kwani wanaendelea kukumbwa na makali ya njaa kila mara kunapokuwa na uhaba wa mvua.

Serikali kuu na ya kaunti zilikuwa zimewekeza mamilioni ya pesa kuanzisha miradi iliyolenga kuwasaidia wakulima wadogo kuzalisha mazao mashambani mwao wakati wa msimu wa kiangazi.

Maeoebunge ya Ganze na Magarini ndiyo yameathirika zaidi kwa uhaba wa njaa mwaka huu, kwa mujibu wa ripoti za serikali za kaunti zinazoonyesha pia kuna uhaba mkubwa wa maji.

Katika baadhi ya maeneo ya Ganze, wakazi wameripoti vifo vya mifugo wao ambao wamekosa malisho.

Wiki chache zilizopita, machifu na viongozi wengine wa serikali kuu katika kaunti hiyo walitoa wito kwa wahisani kuingilia kati ili kuepusha maafa ya wakazi wanaokumbwa na njaa.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Kilifi, Bw Baha Nguma, alithibitisha kuwa Sh28 milioni zilikuwa zimetumiwa katika mojawapo ya miradi ya kunyunyizia maji mashamba madogo eneo la Burangi.

Mradi huo ulilenga jumla ya ekari 3,000 za mashamba.Miradi mingine kama hiyo ilinuiwa kuanzishwa katika maeneo ya Mudachi, Mangudho, Dagamra, Balagha na Sabaki.

Kulingana naye, mradi wa kunyunyiza maji mashambani uliharibiwa na mafuriko kati ya mwaka wa 2016 na 2017.

Mwenyekiti wa mradi wa Mudachi, Bw Edward Mwagandi, alisema mradi huo ulitumiwa kwa misimu miwili pekee.Alieleza kuwa, hata katika msimu huo, idadi kubwa ya wakulima hawakujua kuhusu jinsi ya kunyunyiza maji mashambani.

Kando na hayo, mimea ambayo ilipandwa shambani iliharibiwa na wadudu na maradhi mengine ya mimea.

“Tulikuwa tumefurahi kwa sababu tulitumai kuzalisha chakula kingi ambacho kingenufaisha jamii pamoja na watu wanaotoka nje ya eneo hili lakini mradi ukasambaratika kabla tufaidike kutokana nao,” akasema.

Alidai kuwa, kando na jinsi wakulima hawakujua jinsi ya kutumia mradi huo, ujenzi wake ulifanywa kwa njia duni na hivyo kufanya maji kuvuja bila kufika mashambani ipasavyo.

“Tuliambiwa serikali ya kaunti ilikuwa imetenga Sh6 milioni kwa ujenzi wa mitaro ambayo ingefikisha maji mashambani, lakini ujenzi ulikuwa duni na wakulima wakashindwa kudhibiti viwango vya maji,” akaeleza.

Afisa Mkuu wa Kilimo katika Kaunti ya Kilifi, Bw Victor Nzai, alisema usimamizi mbaya wa mradi huo ndio ulifanya usambaratike.

Kulingana naye, ukosefu wa ujuzi kwa wakulima ulikuwa changamoto kubwa na hapakuwepo maafisa wa kutosha kutoa mafunzo hayo.

“Mradi haukutekelezwa vyema kwa sababu ujenzi wa miundomsingi haukuwa sawa jinsi ilivyokusudiwa,” akasema.

Kitaifa, kuna kaunti 12 ambazo zimetajwa kuwa wakazi wamo hatarini kuathirika na njaa hadi Desemba.

Hali hii imesababishwa na jinsi kulivyokuwa na uhaba wa mvua mwaka uliopita na vile vile katika msimu wa mvua mwaka huu 2021.

You can share this post!

Hichilema aapishwa huku raia wakitarajia mwamko mpya

Uhuru asimamisha jaji kazi