Man-City kuanza kutetea ubingwa wa EPL kwa kibarua kizito katika mechi saba za kwanza za msimu mpya wa 2021-22

Man-City kuanza kutetea ubingwa wa EPL kwa kibarua kizito katika mechi saba za kwanza za msimu mpya wa 2021-22

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi Manchester City watafungua kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2021-22 kwa kumenyana na Tottenham Hotspur ugenini.

Mechi za raundi ya kwanza katika msimu mpya wa EPL zitasakatwa Agosti 14. Limbukeni Brentford waliopandishwa ngazi kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) mwishoni mwa 2020-21 watakuwa wenyeji wa Arsenal. Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Brentford kushiriki tangu 1946-47.

Norwich City na Watford ambao pia walipandishwa ngazi kushiriki EPL mwishoni mwa muhula wa 2020-21, watamenyana na Liverpool na Aston Villa mtawalia.

Manchester United wataanza kuwania taji la kipute hicho kwa kupepetana na Leeds United uwanjani Old Trafford huku wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Chelsea, wakialika Crystal Palace ugani Stamford Bridge.

Vikosi vya EPL viliruhusu mechi za mwisho wa msimu wa 2020-21 kuhudhuriwa na idadi ndogo ya mashabiki baada ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona kulegezwa.

Kufikia sasa, bado haijajulikana iwapo mashabiki wataruhusiwa uwanjani kwa ajili ya msimu mpya wa 2021-22. Iwapo watakubaliwa, basi hata mpangilio utakaotumiwa bado haujafichuliwa na waratibu wa kipute cha EPL japo wamesisitiza kwamba azma yao ni kushuhudia mashabiki wa klabu za nyumbani na ugenini wakianza kujaza viwanja.

Ingawa Man-City wanaonolewa na kocha Pep Guardiola wanapigiwa upatu wa kuhifadhi ubingwa wa EPL, kikosi hicho kitaanza kutetea taji kwa kibarua kigumu dhidi ya Tottenham, Norwich, Arsenal, Leicester, Southampton, Chelsea na Liverpool kwa usanjari huo.

Baada ya kumenyana na Liverpool, Norwich waliorejea EPL baada ya kukaa nje kwa msimu mmoja pekee, watapepetana na Man-City, Leicester na Arsenal katika michuano mitatu itakayofuata.

Gozi la kwanza la London Derby kati ya Tottenham na Arsenal litatandazwa Septemba 25 huku Everton wakialika Liverpool kwa mkondo wa kwanza wa Merseyside Derby mnamo Novemba 30 uwanjani Goodison Park.

Man-United watakuwa wenyeji wa Man-City kwenye mkondo wa kwanza wa gozi la jiji la Manchester mnamo Novemba 11 uwanjani Old Trafford kabla ya Liverpool kuvaana na Leeds nao Man-City kupimana ubabe na Leicester mnamo Disemba 26, 2021.

Mechi za raundi ya pili kutoka mwisho zitasakatwa Mei 15 baada ya fainali ya Kombe la FA kupigiwa Mei 14. Mechi zote 10 za mwisho wa kampeni za msimu wa 2021-22 zimeratibiwa kutanadazwa Mei 22.

MECHI ZA RAUNDI YA KWANZA 2021-22:

Brentford na Arsenal

Burnley na Brighton

Chelsea na Crystal Palace

Everton na Southampton

Leicester City na Wolves

Man-United na Leeds United

Newcastle United na West Ham

Norwich City na Liverpool

Tottenham na Man-City

Watford na Aston Villa

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kocha Benitez pazuri zaidi kuwa mrithi wa Ancelotti kambini...

Italia wakung’uta Uswisi na kuingia hatua ya 16-bora...