Man-City kuvaana na Spurs kwenye fainali ya Carabao Cup baada ya kudengua Man-United kwenye nusu-fainali

Man-City kuvaana na Spurs kwenye fainali ya Carabao Cup baada ya kudengua Man-United kwenye nusu-fainali

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walinusia ubingwa wa taji la Carabao Cup kwa mara nyingine baada ya kuwapepeta Manchester United 2-0 mnamo Jumatano na kufuzu kwa fainali itakayowakutanisha na Tottenham Hotspur uwanjani Wembley mnamo Aprili 25, 2021.

Spurs walijikatia tiketi ya fainali ya Carabao Cup baada ya kucharaza Brentford 2-0 kwenye nusu-fainali ya kwanza mnamo Januari 5, 2021.

Kikubwa zaidi kinachotarajiwa kuchangia motisha ya Man-City ya kocha Pep Guardiola kwenye fainali ya msimu huu ni msukumo wa kutaka kuweka rekodi ya kutwaa taji la Carabao Cup kwa msimu wa nne mfululizo.

Mabao yote mawili ya Man-City yalifumwa wavuni katika kipindi cha pili kupitia beki John Stones na kiungo mkabaji Fernandinho.

Bao la Stones lilitokana na frikiki iliyochanjwa na chipukizi Phil Foden katika dakika ya 50. Ingawa goli hilo liliwazindua Man-United walioanza kushambulia zaidi kupitia Anthony Martial, Marcus Rashford, Aaron Wan-Bissaka na Bruno Fernandes, juhudi zao hazikuzaa matunda yoyote langoni mwa kipa Zach Steffen aliyejaza nafasi ya Ederson Moraes wa Man-City.

Badala yake, ni Fernandinho aliyejaza mpira kimiani mwa Man-United baada ya kuvurumisha kombora kutoka hatua ya 20 na kumwacha hoi kipa Dean Henderson katika dakika ya 83.

Man-City wataifikia rekodi ya Liverpool iwapo watacharaza Spurs na kutia kibindoni ufalme wa Carabao Cup kwa mara ya nne mfululizo.

Mechi hiyo itakuwa fainali ya kwanza tangu 2011 kuwahi kukutanisha kocha Guardiola na Jose Mourinho. Mnamo 2011, Mourinho ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Spurs, aliongoza Real Madrid ya Uhispania kuwanyima Barcelona wa Guardiola fursa ya kutwaa mataji matatu kwa mkupuo kwa kuwapiga kwenye fainali ya Copa del Rey.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United kwa sasa wamepoteza nusu-fainali nne ya mapambano ya kuwania vikombe mbalimbali katika soka ya Uingereza na bara Ulaya chini ya kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Mechi kati Man-United na Man-City ulitoa fursa ya kikosi cha Guardiola kumwomboleza aliyekuwa jagina wao wa soka, Colin Bell aliyeaga dunia mnamo Januari 5, 2021 akiwa na umri wa miaka 75.

Bell alikuwa sehemu ya kikosi cha Man-City kilichotwaa taji la League Cup mnamo 1970 baada ya kufunga bao dhidi ya Man-United kwenye nusu-fainali.

Joao Cancelo, Raheem Sterling na Riyad Mahrez walipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo zingewavunia Man-City mabao zaidi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Katika msimu wa 2019-20, Man-City waliwabandua Man-United kwenye nusu-fainali ya mikondo miwili ya EFL Cup. Baadaye, kikosi hicho cha Solskjaer kiling’olewa na Chelsea kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA kabla ya Sevilla ya Uhispania kuwadengua kwenye nusu-fainali nyingine ya Europa League.

Hiyo ni rekodi mbovu kwa Solskjaer ambaye ni raia wa Norway ikizingatiwa kwamba kocha Sir Alex Ferguson aliyestaafu mnamo 2013, alipoteza nusu-fainali sita pekee kati ya 26 katika enzi yake ya ukufunzi ugani Old Trafford.

Man-United walikosa huduma za fowadi Edinson Cavani dhidi ya Man-City mnamo Jumatano kwa kuwa nyota huyo raia wa Uruguay angali anatumikia marufuku ya mechi tatu baada ya kuadhibiwa na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kwa utovu wa nidhamu mwishoni mwa mwaka wa 2020.

Man-United kwa sasa watakuwa wenyeji wa Watford kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 9 huku Man-City wakivaana na Birmingham City kwenye Kombe la FA siku moja baadaye ugani Etihad.

You can share this post!

Pochettino aanza kazi ya ukocha PSG kwa sare dhidi ya...

Miamba Atletico Madrid watolewa mapema kwenye kivumbi cha...