Man-City sasa wanahitaji alama nane pekee kutokana na mechi tano zilizosalia ili kutwaa ufalme wa EPL msimu huu

Man-City sasa wanahitaji alama nane pekee kutokana na mechi tano zilizosalia ili kutwaa ufalme wa EPL msimu huu

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliwapepeta Aston Villa 2-1 ugenini mnamo Jumatano na kuweka mkono mmoja kwenye taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Vikosi vyote viwili vilikamilisha mchuano huo na wachezaji 10 uwanjani. Hii ni baada ya beki John Stones wa Man-City kufurushwa uwanjani katika dakika ya 44 naye Matty Cash akitimuliwa kunako dakika ya 55 baada ya kuonyeshwa kadi mbili za manjano chini ya kipindi cha sekunde 180. Stones aliadhibiwa kwa kosa la kumchezea visivyo kiungo Jacob Ramsey.

Man-City walikuwa wakicheza kwa mara ya kwanza tangu kutangaza kujiunga na kipute kipya cha European Super League (ESL) kisha kujiondoa tena kwenye mashindano hayo saa 24 baadaye.

Villa waliwekwa uongozini dhidi ya Man-City na fowadi John McGinn katika dakika ya 20 baada ya kushirikiana vilivyo na mshambuliaji Ollie Watkins na kumwacha hoi kipa Ederson Moraes.

Hata hivyo, kiungo mvamizi Phil Foden aliwarejesha Man-City mchezoni kunako dakika ya 22 kabla ya Rodri kukamilisha krosi ya Bernardo Silva kirahisi na kufungia waajiri wake goli la ushindi katika dakika ya 40.

Chini ya mkufunzi Pep Guardiola, Man-City kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 77 huku pengo la pointi 11 likitamalaki kati yao na nambari mbili Manchester United.

Kikosi hicho kinachofukuzia pia mataji ya Carabao Cup na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, sasa kinahitaji kujizolea alama nane pekee kutokana na mechi tano zilizosalia ili kutawazwa mabingwa wa EPL kwa mara ya tatu chini ya kipindi cha misimu minne.

Stones atakosa sasa fainali ya Carabao Cup itakayowakutanisha Man-City na Tottenham Hotspur uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Aprili 25, 2021. Man-City pia wametinga nusu-fainali za UEFA ambapo watavaana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa katika mkondo wa kwanza mnamo Aprili 28 ugenini kabla ya kurudiana wiki moja baadaye uwanjani Etihad, Uingereza.

Villa ambao kwa sasa wanakamata nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 44, wamepangiwa kuchuana na West Bromwich Albion katika mchuano wao ujao wa EPL mnamo Aprili 25, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mashabiki wa Schalke washambulia kikosi kwa mayai baada ya...

Vissel na Sagan walimwa Ayub Timbe na Ismael Dunga wakila...