Man-City wacharaza Burnley tena na kujiweka pazuri kutwaa taji la EPL msimu huu

Man-City wacharaza Burnley tena na kujiweka pazuri kutwaa taji la EPL msimu huu

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walifungua mwanya wa alama tatu kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Februari 3, 2021 baada ya kupiga Burnley 2-0 ugani Turf Moor na kuendeleza rekodi ya kushinda kikosi hicho cha kocha Sean Dyche mara 13 mfululizo.

Awali, ushindi wa 9-0 uliosajiliwa na Manchester United dhidi ya Southampton ulishuhudia Man-City wakitoshana alama na watani wao hao japo masogora wa kocha Pep Guardiola wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na washindani wao wakuu wakiwemo Man-United, Leicester City, Liverpool na West Ham United.

Man-City walifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya tatu kupitia kwa Gabriel Jesus aliyechuma nafuu kutokana na masihara ya kipa Nick Pope aliyeshindwa kudhibiti ipasavyo kombora aliloelekezewa na Bernardo Silva.

Licha ya kuchezea ugenini, Man-City walitamalaki mchezo na kuwazidi maarifa wenyeji wao katika kila idara huku wakimiliki asilimia kubwa ya mpira. Man-City wanaopigiwa upatu kutwaa ubingwa wa EPL msimu huu, walipachika wavuni bao lao la pili katika dakika ya 38 kupitia kwa Raheem Sterling aliyeshirikiana vilivyo na kiungo Ilkay Gundogan.

Bao la Riyad Mahrez aliyefunga Burnley mabao matatu katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Novemba 2020 lilikataliwa kwa madai kwamba alikuwa ameotea. Burnley hawakuelekeza kombora lolote langoni pa Man-City.

Matokeo hayo yalishuhudia Burnley wakishuka hadi nafasi ya 17 jedwalini kwa alama 22 sawa na Newcastle United. Fulham waliopigwa na Leicester City 2-0 wako katika orodha ya vikosi vitatu vya mwisho kwa pamoja na West Bromwich Albion na Sheffield United.

Kutokuwepo kwa Kevin de Bruyne anayeuguza jeraha kulimpa Gundogan fursa ya kutamba kwenye safu ya kati huku ushirikiana wake na Silva ukimwezesha Sterling kufunga bao lake la 10 kufikia sasa msimu huu.

Man-City walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo wakijivunia rekodi ya kupiga Burnley 5-0 mara nne katika kipindi cha miaka mitatu ya awali.

Burnley kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Brighton watakaoshuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo ya Februari 6 wakijivunia motisha ya kupiga Liverpool 1-0 mnamo Februari 3 uwanjani Anfield.

Kwa upande wao, Man-City watakuwa na kibarua kizito cha kuangusha Liverpool uwanjani Anfield mnamo Februari 7. Ushindi kwa Man-City katika gozi hilo dhidi ya masogora wa kocha Jurgen Klopp huenda ukawaweka pazuri zaidi kutwaa ubingwa wa EPL msimu huu.

MATOKEO YA EPL (Februari 3):

Burnley 0-2 Man-City

Fulham 0-2 Leicester City

Leeds 1-2 Everton

Aston Villa 1-3 West Ham Utd

Liverpool 0-1 Brighton

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mbappe na Di Maria wasaidia PSG kuendeleza presha kwa Lille

Olunga nje ya Kombe la Dunia la Klabu