Man-City wakomoa Aston Villa ugani Etihad na kuhifadhi taji la EPL

Man-City wakomoa Aston Villa ugani Etihad na kuhifadhi taji la EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walitoka nyuma kwa mabao mawili na kukomoa Aston Villa 3-2 mnamo Jumapili ugani Etihad katika ushindi uliowawezesha kuhifadhi taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Man-City walijikuta chini kwa mabao 2-0 kufikia dakika ya 15 ila wakarejea mchezoni kupitia kwa Ilkay Gundogan aliyetokea benchi na kufunga mabao mawili kabla ya Rodri kupachika wavuni goli la ushindi.

Taji hilo la EPL lilikuwa la nne kwa Man-City kuzoa chini ya misimu mitano na la 11 kwa Guardiola kutwaa katika kipindi cha miaka sita ya ukufunzi wake nchini Uingereza.

“Ushindi huu umechangiwa na ubora wa wachezaji wetu. Isitoshe, uchochewa zaidi na ushindani mkali kutoka kwa Liverpool. Ilikuwa fahari tele kunyanyua taji mbele ya mashabiki wetu wa nyumbani,” akasema Guardiola.

Ilikuwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 17 kwa Man-City kutoka chini kwa mabao mawili na kushinda mechi ligini. Katika msimu wake wa pili ugani Etihad, Mhispania huyo alinyanyua ubingwa wa EPL mnamo 2017-18 kabla ya kulihifadhi 2018-19. Man-City walitwaa ubingwa wa msimu huu siku chache baada ya wanasoka wao wawili – Kevin de Bruyne na Phil Foden – kutawazwa Mchezaji Bora na Chipukizi Bora mtawalia katika EPL.

Miamba hao walifunga msimu kwa kujizolea alama 93, moja zaidi kuliko nambari mbili Liverpool waliokomoa Wolverhampton Wanderers 3-1 ugani Anfield. Walitamalaki michuano 29, kutoka sare mara sita na kulazwa mara tatu pekee kutokana na mechi 38 ligini. Liverpool wanaofukuzia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na la tatu msimu huu, walishinda mechi 28, kuambulia sare mara nane na kupoteza michuano miwili.

“Sisi ni manguli. Tutakumbukwa. Sifa za kundi hili la wachezaji wa Man-City zitadumu kwa miaka na mikaka,” akaongeza Guardiola.

“Ni vigumu sana kupata mafanikio haya. Sir Alex Ferguson aliwahi kufikia ufanisi huu mara mbili au tatu akidhibiti mikoba ya Manchester United. Nimejua ugumu wa kibarua alichokuwa nacho,” akasisitiza.

Ushindi wa Man-City unatarajiwa kumchochea Guardiola kurefusha muda wa kuhudumu kwake ugani Etihad ikizingatiwa kuwa mkataba wake wa sasa na mabingwa hao mara sita wa EPL unatamatika mwisho wa msimu ujao.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Arsenal 5-1 Everton

Brentford 1-2 Leeds United

Brighton 3-1 West Ham Utd

Burnley 1-2 Newcastle

Chelsea 2-1 Watford

Palace 1-0 Man-Utd

Leicester 4-1 Southampton

Liverpool 3-1 Wolves

Man-City 3-2 Aston Villa

Norwich 0-5 Tottenham

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Pigo kwa Chris Wamalwa kambi ya Natembeya ikipigwa jeki

Twaha Mbarak akutana na Origi Anfield baada ya Liverpool...

T L