Michezo

Man-City wampa Fernandinho unahodha wa timu

September 21st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City tayari wamejinasia huduma za wanasoka wawili muhula huu – mvamizi Ferran Torres kutoka Uhispania na beki Nathan Ake ambaye ni raia wa Uholanzi.

Ake aliyetokea Bournemouth atachezeshwa kwa mara ya kwanza na Man-City mnamo Septemba 21 baada ya Guardiola kuthibitisha kwamba atajaza nafasi ya Aymeric Laporte aliyekosa vipindi kadhaa zilivyopita vya mazoezi tangu augue Covid-19.

Guardiola amefichua maazimio ya kumsajili beki mwingine wa kulia atakayempiga jeki Fernandinho ambaye sasa amepokezwa utepe wa unahodha. Fernandinho ambaye ni raia wa Brazil, anatwaa majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na kiungo David Silva.

Fernandinho ameidhinishwa kuwa kapteni wa Man-City baada ya kupendekezwa na idadi kubwa ya wanasoka wenzake ugani Etihad.

Baada ya kuagana na Man-City mwishoni mwa msimu wa 2019-20, Silva aliyoyomea kambini mwa Real Sociedad waliomsajili kwa mkataba wa miaka miwili.

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 34 alitamatisha kipindi cha miaka 10 cha kuvalia jezi za Man-City mnamo Agosti 15, 2020 katika mechi iliyowashuhudia waliokuwa waajiri wake wakibanduliwa na Olympique Lyon ya Ufaransa kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) jijini Lisbon, Ureno.

Silva ambaye alisajiliwa na Man-City kutoka Valencia mnamo 2010, aliwajibishwa uwanjani Etihad katika jumla ya mechi 436 na akasaidia kikosi hicho kunyanyua jumla ya mataji 14.

Aliteua kuingia katika sajili rasmi ya Sociedad baada ya kukataa ofa ya Inter Miami ya Amerika na Lazio ya Italia iliyokuwa radhi kumpokeza mkataba wa miaka mitatu.

Sociedad walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu uliopita katika nafasi ya sita jedwalini na walijipata katika ulazima wa kutafuta mwanasoka kizibo cha Martin Odegaard aliyerejea Real Madrid baada ya kipindi chake cha mkopo kambini mwa Sociedad kutamatika.

Akivalia jezi za Man-City, Silva aliwajibishwa katika mechi 309 za EPL ambapo alifunga mabao 60 na akachangia pakubwa mafanikio ya kikosi hicho kutwaa mataji manne ya EPL mnamo 2012, 2014, 2018 na 2019.

Katika mechi nyinginezo zisizokuwa za EPL na UEFA, alichezeshwa na Man-City mara 57 na akasaidia kikosi hicho kutwaa makombe mawili ya FA, matano ya League Cup na matatu ya Community Shield.

Silva anashikilia rekodi ya kuwa mwanasoka anayejivunia kusakatia Man-City idadi kubwa zaidi ya mechi (70) kwenye UEFA chini ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Uhispania kilichonyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2010 na mataji ya Euro mnamo 2008 na 2012. Msimu mpya wa 2020-21 katika La Liga umeratibiwa kuanza Septemba 12, 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO