Man-City wang’aria Club Brugge huku chipukizi Cole Palmer akiweka rekodi ya ufungaji katika soka ya UEFA

Man-City wang’aria Club Brugge huku chipukizi Cole Palmer akiweka rekodi ya ufungaji katika soka ya UEFA

Na MASHIRIKA

RIYAD Mahrez alifunga mabao mawili katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ulioshuhudia waajiri wake Manchester City wakikung’uta Club Brugge ya Ubelgiji 5-1 mnamo Jumanne.

Mechi hiyo ilitoa jukwaa mwafaka kwa chipukizi Cole Palmer kufungia Man-City ya kocha Pep Guardiola bao la kwanza katika soka ya UEFA.

Ushindi wa Man-City ambao ulikuwa wao wa pili kwenye UEFA msimu huu, uliwadumisha katika nafasi ya pili kwenye Kundi A kwa alama sita, moja nyuma ya viongozi Paris Saint-Germain (PSG). Club Bruges wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi nne huku RB Leipzig wakivuta mkia bila alama yoyote.

Licha ya kutamalaki mchezo na kuwazidi wenyeji wao maarifa katika takriban kila idara, Man-City walilazimika kusubiri hadi dakika ya 30 kufungua ukurasa wa mabao kupitia Joao Cancelo aliyekamilisha krosi ya Phil Foden ambaye pia alimtatiza pakubwa kipa Simon Mignolet.

Mahrez alifunga bao la pili kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya 43 kabla ya ushirikiano kati yake na Kevin de Bruyne kuchangia goli la tatu ambalo Man-City walifungiwa na Kyle Walker katika dakika ya 53.

Palmer, 19, alicheka na nyavu za Club Bruges katika dakika ya 67, sekunde chache baada ya kuletwa uwanjani. Mahrez alifungia Man-City bao la tano katika dakika ya 83, dakika tatu baada ya Hans Vanaken kufutia Clu Bruges machozi.

Man-City walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi baada ya PSG kuwapepeta 2-0 katika mechi ya awali mnamo Septemba 28, 2021.

Palmer aliyekwezwa hadi kikosi cha kwanza cha Man-City kutoka akademia msimu huu, ndiye mwanasoka wa tatu wa umri mdogo zaidi baada ya Foden na Kelechi Iheanacho ambaye sasa anachezea Leicester City kuwahi kufungia Man-City bao kwenye kampeni za UEFA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Washukiwa kusalia seli siku 10

Salah avunja rekodi ya ufungaji wa mabao ya UEFA kambini...

T L