Michezo

Man-City watoka sare na Porto na kukamilisha kampeni za Kundi C kileleni

December 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LICHA ya kuambulia sare tasa dhidi ya FC Porto ugenini, Manchester City wana uhakika wa kukamilisha kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu kileleni mwa Kundi C.

Bao ambalo masogora hao wa kocha Pep Guardiola walifungiwa na fowadi Gabriel Jesus mwishoni mwa kipindi cha pili lilifutiliwa mbali na refa kwa mAdai kwamba lilifumwa wavuni wakati Joao Cancelo alikuwa ameotea.

Man-City waliingia ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakitawaliwa na hamasa ya kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakiwafunga Burnley 5-0 katika mchuano wa awali wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Hata hivyo, mashabulizi yao yalidhibitiwa vilivyo na mabeki watano wa Porto chini ya uongozi wa Zaidu Sanusi, huku kipa raia wa Argentina, Agustin Marchesin akifanya kazi ya ziada kupangua makombora ya Raheem Sterling, Ferran Torres, Phil Foden, Bernardo Silva na Jesus.

Alama moja iliyotiwa kapuni na Porto katika mechi hiyo iliwashuhudia pia wakifuzu kwa hatua ya 16-bora katika UEFA msimu huu. Hii ni baada ya Olympique Marseille kuwapepeta Olympiakos 2-1 nchini Ufaransa katika mchuano mwingine wa Kundi C. Marseille na Olympiakos kwa sasa wanajivunia alama tatu kila mmoja.

Guardiola aliwapanga wanasoka wake wa haiba dhidi ya Porto akisisitiza kwamba hatua hiyo ilichochewa na ugumu wa kibarua ambacho miamba hao wa Ureno waliwalazimishia katika mchuano wa mkondo wa kwanza ambao Man-City walishinda 3-1 ugani Etihad mnamo Oktoba, 2020.

Porto kwa sasa hawajasajili ushindi wowote kutokana na mechi sita zilizopita za UEFA dhidi ya mpinzani kutoka Ligi Kuu ya Uingereza. Kikosi kimeambulia sare mara mbili na kupoteza michuano minne huku kikikosa kufunga bao kutokana na mechi nne kati ya hizo sita.

Man-City kwa sasa wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA kwa msimu wa tano mfululizo wakiwa washindi wa makundi yao katika kipindi cha misimu mitano iliyopita. Mara ya pekee ambapo wamewahi kutinga hatua ya mwondoano wakiwa nambari mbili kundini ni 2016-17 ambapo walikamilisha kampeni za kufuzu nyuma ya miamba wa Uhispania, Barcelona.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kwa mchuano wa EPL utakaowakutanisha na limbukeni Fulham mnamo Disemba 5, 2020 uwanjani Etihad.