EPL: Man-City watuma onyo kali kwa washindani wakuu ligini msimu huu

EPL: Man-City watuma onyo kali kwa washindani wakuu ligini msimu huu

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amekiri kwamba kikosi chake cha Manchester City sasa kiko katika hali shwari zaidi na ushindi wa 3-1 dhidi ya Watford katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi ni mwanzo wa makuu kutoka kwao muhula huu.

Ushindi wa Man-City uliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali la EPL kwa mara ya kwanza msimu huu na kuwaweka pazuri zaidi kuhifadhi ufalme wa kipute hicho kinachotawaliwa na ushindani mkali.

Raheem Sterling aliwaweka Man-City kifua mbele baada ya kukamilisha krosi safi aliyoandaliwa na Phil Foden katika dakika ya nne ya mchezo.

Bao hilo liliwapa Man-City motisha na wangalipachika wavuni mabao zaidi ila kipa Daniel Bachmann akajituma vilivyo na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa.

Masogora wa Guardiola walifungiwa mabao mawili na Bernardo Silva katika dakika za 31 na 63 kabla ya Cucho Hernandez kurejesha Watford mchezoni katika dakika ya 74.

Baada ya kutandaza jumla ya michuano 15 ya EPL msimu huu, Man-City wanaojivunia kutwaa taji la EPL mara tano katika kipindi cha misimu 10 iliyopita, sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 35, moja zaidi kuliko nambari mbili Liverpool.

Chelsea walishuka hadi nambari ya tatu baada ya West Ham United wanaokamata nafasi ya nne kuwapokeza kichapo cha 3-2 ugani London.

Kwa upande wa Watford, kichapo kutoka kwa Man-City kilikuwa chao cha sita kutokana na mechi nane zilizopita chini ya kocha Claudio Ranieri ambaye amewaongoza kumenyana na vikosi vitano kati ya saba vinavyodhibiti kilele cha jedwali kwa sasa.

Japo Watford walipepeta Everton 5-2 na kupiga Manchester United 4-1 katika mchuano wa mwisho kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer kambini mwa Red Devils, masogora wa Ranieri wamejizolea alama sita pekee ligini tangu mkufunzi Xisco Munoz atimuliwe ugani Vicarage Road mnamo Oktoba 2021.

Watford kwa sasa wanashikilia nafasi ya 17 jedwalini kwa alama 13, tatu zaidi kuliko Burnley, Newcastle United na Norwich City wanaokamata nafasi tatu za mwisho kwenye orodha ya washiriki wa EPL muhula huu.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

West Ham 3-2 Chelsea

Newcastle 1-0 Burnley

Southampton 1-1 Brighton

Wolves 0-1 Liverpool

Watford 1-3 Man-City

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Origi abeba Liverpool dhidi ya Wolves ligini

Wadudu waharibifu wavamia mashamba ya mahindi Gatundu...

T L