Man-City watwanga Wolves na kufungua pengo la alama 15 kileleni mwa jedwali la EPL

Man-City watwanga Wolves na kufungua pengo la alama 15 kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amepongeza wanasoka wake kwa kujituma vilivyo na kusajili matokeo ya kuridhisha katika kipindi ambapo walikuwa wakikabiliwa na ratiba ngumu.

Ushindi wa 4-1 uliovunwa na viongozi hao wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Wolves mnamo Jumanne usiku ulikuwa wao wa 21 mfululizo kwenye mashindano yote kufikia sasa msimu huu.

Mabingwa hao wa zamani wa EPL walifunga mabao matatu ya haraka chini ya kipindi cha dakika 10 za mwisho wa mchuano uliowakutanisha na Wolves ya mkufunzi Nuno Espirito.

Man-City kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote tangu walazimishiwe sare na West Bromwich Albion mnamo Disemba 15. Kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 65 huku pengo la pointi 15 likitamalaki kati yao na nambari mbili Manchester United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Katika kipindi hicho cha michuano 21 iliyopita, Man-City walitinga fainali ya League Cup, robo fainali za Kombe la FA na kujiweka pazuri kuingia robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kupiga Borussia Monchengladbach ya Ujerumani 2-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora mnamo Februari 24, 2021.

Miamba hao wa soka ya Uingereza sasa watakutana na Tottenham Hotspur kwenye fainali ya Carabao League Cup mnamo Aprili 25 ugani Wembley, Uingereza baada ya kuchuana na Everton kwenye mikondo miwili ya robo-fainali za Kombe la FA.

Wakicheza dhidi ya Wolves, Man-City waliweka uongozini na Leander Dendoncker aliyejifunga mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Conor Coady kusawazisha mambo. Mabao mengine ya Man-City katika mechi hiyo yalifumwa wavuni na Gabriel Jesus na Riyad Mahrez aliyefunga lake la saba kufikia sasa ligini msimu huu.

Man-City wanajiandaa sasa kupepetana na Man-United ugani Etihad mnamo Machi 7, 2021 katika mchuano utakaowapa jukwaa la kuajili ushindi wa 16 mfululizo ligini na wa 22 kutokana na mechi zote za hadi kufikia sasa muhula huu.

“Tuna muda mfupi wa kupumzika kabla ya kushuka dimbani kwa mechi ngumu. Ni mechi itakayotia kwenye mizani uwezo wetu wa kutwaa ubingwa wa EPL msimu huu. Tunatarajia kusajili matokeo ya kuridhisha hasa baada ya ratiba ngumu iliyotutia kigezoni,” akasema kocha huyo raia wa Uhispania ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Wolves kwa upande wao watakuwa wageni wa Aston Villa katika mechi yao ijayo ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mwanamke adai Mungu alimtuma kumumunya Sh30 milioni katika...

Mtambue mtangazaji wa soka chipukizi ‘Arocho’