Man-City wazamisha West Ham tena na kuendeleza ubabe wao katika EPL

Man-City wazamisha West Ham tena na kuendeleza ubabe wao katika EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliendeleza ubabe wao katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kutandika West Ham United 2-1 mnamo Jumapili ugani Etihad.

Mechi hiyo ilikuwa ya 10 kati ya 11 zilizopita kwa Man-City kushinda dhidi ya West Ham chini ya kocha Pep Guardiola ligini.

Ilkay Gundogan aliwaweka Man-City kifua mbele baada ya kukamilisha krosi ya Riyad Mahrez katika dakika ya 33.

Bao hilo lilikuwa la tatu kwa kiungo raia wa Ujerumani kufungia Man-City muhula huu na la pili kutokana na mechi nne zilizopita za EPL. Goli la pili la Man-City lilipachikwa wavuni na Fernandinho kabla ya West Ham ya kocha David Moyes kufutiwa machozi na Manuel Lanzini mwishoni mwa kipindi cha pili.

Bao la Fernandinho lilikuwa lake la kwanza katika EPL tangu Oktoba 2018. Kipa Ederson Moraes wa Man-City alipania kuweka rekodi ya kutofungwa katika mechi 100 katika mashindano yote. Hata hivyo, Lanzini alivuruga azma yake hiyo.

Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa EPL sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 29, moja pekee nyuma ya Chelsea. West Ham kwa upande wao wanakamata nafasi ya nne kwa alama 23 sawa na Arsenal wanaofunga orodha ya tano-bora. Ilikuwa mara ya kwanza tangu Aprili 2021 kwa West Ham kupoteza mechi mbili mfululizo kwenye EPL.

West Ham wamepoteza mechi 22 kati ya 25 zilizopita dhidi ya Man-City katika EPL ugenini. Man-City kwa sasa wanajiandaa kumenyana na Aston Villa ugenini katika mechi ya EPL mnamo Disemba 1, 2021 huku West Ham wakialika Brighton uwanjani London Stadium.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kipusa Viviane Miedema atawazwa Mwanasoka Bora wa Kike...

WANTO WARUI: Serikali itoe mwelekeo kuhusu elimu ya juu ya...

T L