Michezo

Man-City yakomoa Southampton na kukaribia ndani ya mduara wa 4-bora EPL

December 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walijongea ndani ya mduara wa nne-bora kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Disemba 19, 2020, baada ya kuwapokeza Southampton kichapo cha 1-0 uwanjani St Mary’s.

Bao hilo la pekee katika mechi hiyo lilipachikwa wavuni na fowadi Raheem Sterling aliyekamilisha kwa ustadi krosi ya kiungo Kevin de Bruyne baada ya dakika 16.

Juhudi za Southampton za kurejea mchezoni na kulazimisha sare katika mechi hiyo ziliambulia pakavu baada ya mshambuliaji wao tegemeo, Danny Ings kupata jeraha lililomlazimu kuondolewa uwanjani kabla ya mwisho wa kipindi cha kwanza.

Bernardo Silva, De Bruyne na Sterling walipoteza nafasi nyingi za wazi za kufungia kikosi chao mabao muhimu katika kipindi cha pili japo kipa wa Southampton, Alex McCarthy alifanya pia kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Ilkay Gundogan.

Man-City walijibwaga ugani kwa minajili ya mchuano huo wakitawaliwa na kiu ya kusajili ushindi baada ya kuambulia sare katika mechi mbili za awali.

Ushindi huo wa Man-City uliwapaisha hadi nafasi ya sita kwa alama 23, moja pekee nyuma ya Southampton.

Ni pengo la alama nane ndilo kwa sasa linatamalaki kati ya Man-City na viongozi wa jedwali Liverpool ambao pia ni mabingwa watetezi wa taji la EPL.

Kutokuwepo kwa Sergio Aguero na Gabriel Jesus katika kikosi cha Man-City kulimweka kocha Pep Guardiola katika ulazima wa kutegemea sajili mpya Ferran Torres huku Ruben Dias akitamba zaidi katika safu ya ulinzi.

Hata hivyo, matatizo ya Man-City yameonekana zaidi kwenye idara ya mbele ambayo imefunga mabao 19 pekee ikilinganishwa na magoli 37 yaliyofumwa na kikosi hicho kutokana na mechi 13 pekee za msimu uliopita wa 2019-20.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Arsenal kwenye robo-fainali za Carabao Cup mnamo Disemba 22 kabla ya kushuka dimbani kupepeta na Newcastle United uwanjani Etihad mnamo Disemba 26, siku ambapo Southampton watawaendea Fulham ugani Craven Cottage.