Michezo

MAN-CITY YANG'ATWA: Wolves yapiga wenyeji mabao 2-0

October 7th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City kwa sasa wameachwa na Liverpool kwa alama nane baada ya kupepetwa Jumapili na Wolves kwa mabao 2-0 uwanjani Etihad.

Adama Traore aliwafungia Wolves mabao yote mawili baada ya kumwacha hoi kipa Ederson Moraes wa Man-City.

Ilikuwa ni mara ya kwanza tangu 1979 kwa Wolves kuwapiga Man-City ambao kwa sasa wamepoteza jumla ya alama tano muhimu katika mechi nne zilizopita ambazo wamechezea nyumbani. Katika kampeni za msimu jana, Man-City walipoteza alama tatu pekee uwanjani Etihad.

Bila kiungo Kevin de Bruyne, Man-City ya kocha Pep Guardiola walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara huku jaribio la Gabriel Jesus langoni pa wenyeji wao likizimwa kirahisi na kipa Rui Patricio ambaye pia alimnyima kiungo Joao Cancelo nafasi mbili za wazi.

Ushindi wa Wolves uliwapaisha jedwalini hadi nafasi ya 11 kwa alama 10, sita zaidi nyuma ya Man-City ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili.

Katika mechi nyingine ya Jumapili, Arsenal walipaa hadi nafasi ya tatu jedwalini baada ya kuwalaza Bournemouth 1-0 uwanjani Emirates.

Chini ya kocha Unai Emery, Arsenal walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wakijivunia hamasa tele baada ya kuwaponda Standard Liege ya Ubelgiji 4-0 katika kivumbi cha awali cha Europa League.

Bao la Arsenal katika mchuano huo wa Jumapili lilifumwa wavuni katika dakika ya tisa kupitia kwa beki David Luiz aliyeingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuagana na Chelsea.

Pengo

Kufikia sasa, ni pengo la alama moja pekee ndilo linalotamalaki kati ya Arsenal na Man-City ambao awali, walipigiwa upatu wa kuzamisha chombo cha Wolves na kuendeleza ushindani mkali dhidi ya Liverpool wanaoselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 24.

Chelsea wanaoanza kuzoea maisha chini ya kocha mpya Frank Lampard waliwasagasaga Southampton 4-1 uwanjani St Mary’s. Tammy Abraham aliwafungulia Chelsea ukurasa wa mabao kunako dakika ya 17 kabla ya chipukizi mwingine Mason Mount kufunga la pili katika dakika ya 24.

Ingawa Danny Ings alipania kuwarejesha Southampton mchezoni katika dakika ya 30, jitihada zake zilifutwa na N’Golo Kante na Michy Batshuayi waliocheka na nyavu kunako dakika ya 40 na 89 mtawalia.

Ushindi wa Chelsea uliwakweza hadi nafasi ya tano kwa alama 14 sawa na Leicester City na Crystal Palace wanaoshikilia nafasi za nne na sita mtawalia. Southampton kwa upande wao kwa sasa wanaorodheshwa wa 16 jedwalini kwa alama saba sawa na Everton.