Michezo

FA: Man City yashikilia ufunguo wa Erik ten Hag kusalia Man U

May 24th, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MATUMAINI ya kocha Erik ten Hag kuendelea kushikilia wadhifa huo katika klabu ya Manchester United yanaonekana kuwa mikononi mwa Manchester City.

Majirani hao watamenyana katika fainali ya Kombe la FA ugani Wembley nchini Uingereza, Jumamosi jioni. Mabingwa watetezi City wanapigiwa upatu kufanya vyema.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka jijini London, Ten Hag kutoka Uholanzi anakabiliwa na presha kali baada ya msimu wa kusikitisha.

United walimaliza ligi katika nafasi ya nane (nafasi mbaya kabisa tangu msimu 1989-1990) na kubanduliwa katika Kombe la Carabao na Klabu Bingwa Ulaya katika raundi ya 16-bora na makundini, mtawalia.

Inasemekana mkurugenzi wa kiufundi wa United Jason Wilcox amefanya utathmini wa kina kuhusu uwezo wa Ten Hag kuendelea katika msimu wa tatu na dalili si nzuri.

Sauti ya mashabiki wa United kutaka kocha huyo wa zamani wa Ajax atimuliwe imekuwa ikiongezeka na kufika kubwa hata zaidi baada ya kichapo cha 4-0 kutoka kwa Crystal Palace mnamo Mei 6.

Ingawa Ten Hag amepuuzilia mbali kuwa fainali ya Kombe la FA dhidi ya City ya kocha Pep Guardiola itakuwa yake ya mwisho kama kocha wa United asiposhinda, inaaminika mmiliki Jim Ratcliffe yuko tayari kufanyia klabu hiyo mabadiliko makubwa ikiwemo katika benchi la kiufundi ili kuleta mwamko mpya ugani Old Trafford.

Iwapo United watafanikiwa kulemea mabingwa wa Ligi Kuu City, basi watapata kufuta aibu na pia tiketi ya kushiriki mashindano ya Ulaya msimu 2024-2025 na pia inakuwa habari nzuri kwa Ten Hag.

Makocha wa zamani wa Chelsea Thomas Tuchel na Mauricio Pochettino wako katika orodha ya makocha wanaopigiwa upatu kujaza nafasi ya Ten Hag akifutwa kazi.