Man-City yaweka hai matumaini ya kutwaa mataji manne baada ya kubomoa Swansea City na kutinga robo-fainali za Kombe la FA

Man-City yaweka hai matumaini ya kutwaa mataji manne baada ya kubomoa Swansea City na kutinga robo-fainali za Kombe la FA

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola alikuwa mwingi wa sifa kwa wachezaji wake wa Manchester baada ya kuwacharaza Swansea City 3-1 kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA uwanjani Liberty mnamo Jumatano na kuweka rekodi mpya kwenye historia ya soka ya Uingerea.

Kyle Walker, Raheem Sterling na Gabriel Jesus walifunga mabao ya Man-City katika gozi hilo na kusaidia waajiri wao kutinga robo-fainali za Kombe la FA msimu huu. Swansea City waliozidiwa maarifa katika kila idara, walifutiwa machozi na mshambuliaji Morgan Whittaker katika dakika ya 77. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Whittaker kuchezeshwa na Swansea katika kikosi cha kwanza.

Mechi hiyo ilikuwa ya 15 mfululizo kwa masogora wa Guardiola kushinda katika mashindano yote ya msimu huu wa 2020-21.

Ushindi huo wa Man-City unamaanisha kwamba kwa sasa wamevunja rekodi iliyowekwa na Preston End mnamo 1891-92 na Arsenal mnamo 1987-88 baada ya kushinda msururu wa mechi 14 mfululizo katika mashindano yote kwenye soka ya Uingereza.

“Inaonyesha jinsi ambavyo wachezaji wangu ni spesheli. Kikubwa zaidi tunacholenga kuepuka ni kupotezewa dira na sifa hizi zinazozidi kutolewa kutuhusu. Najua tumevunja rekodi, nab ado tutavunja nyinginezo. Kufanya hivyo si jambo rahisi. Kunahitaji kujituma na kuweka wazi maazimio yako hata kabla ya kuingia uwanjani,” akasema kocha huyo raia wa Uhispania aliyewahi pia kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Chini ya Guardiola, Man-City bado wanafukuzia jumla ya mataji manne kwenye kampeni za msimu huu. Mbali na Kombe la FA, kikosi hicho kinapigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Carabao Cup.

Man-City hawajawahi kupoteza mchuano wowote tangu Novemba 2020 na walijibwaga ugani kupepetana na Swansea wakijivunia motisha tele ya kuwaponda Liverpool 4-1 katika mechi yao iliyopita ya EPL uwanjani Anfield.

Kufikia sasa, Man-City wamefunga jumla ya mabao 43 na nyavu zao kutikiswa mara 14 pekee kutokana na mechi 22 zilizopita za EPL. Tangu Novemba, kikosi hicho kimefungwa mabao matano pekee.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wachezaji wa Gor Mahia wagoma tena mechi ya CAF ikibisha

Usicheze na Rais – Jenerali