Michezo

Man U wabanwa na West Ham

July 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER United sasa wanahitaji alama moja pekee katika mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Leicester City uwanjani King Power ili kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Hii ni baada ya hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer kutoka nyuma na kusajili sare ya 1-1 dhidi ya West Ham United uwanjani Old Trafford mnamo Julai 22, 2020.

Matokeo hayo yaliwapaisha Man-United hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 63 sawa na Chelsea ambao kwa sasa wanajiandaa kuweka kando maruerue ya kuchapwa 5-3 na Liverpool kabla ya kufunga kampeni zao za muhula huu dhidi ya Wolves ugani Stamford Bridge mnamo Julai 26, 2020.

Ushindi kwa kikosi cha Leicester kinachotiwa makali na mkufunzi Brendan Rodgers utawanyima Man-United nafasi ya kunogesha kivumbi cha UEFA iwapo Chelsea nao watawanyuka Wolves katika gozi la Julai 26.

Alama moja ambayo West Ham ya kocha David Moyes ilijizolea dhidi ya Man-United ilitosha kuwadumisha katika kivumbi cha EPL msimu ujao. Kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya 15 kwa alama 38 sawa na Brighton. Wawili hao wana alama nne zaidi nje ya mduara hatari wa kushuka daraja ambao kwa sasa unamilikiwa na Watford, Bournemouth na Norwich City ambao tayari wameshushwa ngazi.

Michail Antonio aliwaweka West Ham kifua mbele kunako dakika ya 45 kupitia penalti iliyochangiwa na Paul Pogba aliyenawa mpira uliokuwa umepigwa na Declan Rice. Bao hilo lilikuwa lake la nane kutokana na mechi sita zilizopita.

Man-United walisawazishiwa na chipukizi Mason Greenwood, 18, katika dakika ya 51. Bao la kinda huyo lilikuwa lake la 17 kufikia sasa katika mapambano yote ya msimu huu.

Baada ya kusakata jumla ya mechi 19 bila ya kupoteza yoyote, Man-United wamekuwa na wiki mbaya katika soka ya Uingereza baada ya kubanduliwa na Chelsea kwenye nusu-fainali za Kombe la FA uwanjani Wembley kisha kulazimishiwa sare na West Ham katika uga wao wa nyumbani wa Old Trafford.

Kufuzu kwa kivumbi cha UEFA msimu ujao kutawaongezea Man-United ushawishi zaidi wa kujinasia huduma za chipukizi mzawa wa Uingereza, Jadon Sancho ambaye kwa sasa anavalia jezi za Borussia Dortmund nchini Ujerumani.

Baada ya kuweka rekodi ya kutokamilisha kipute cha EPL nje ya mduara wa tatu-bora chini ya kocha Sir Alex Ferguson kwa misimu 22, Man-United wamefaulu kumalizi kampeni za ligi ndani ya orodha ya nne-bora mara mbili pekee tangu kustaafu kwa Ferguson mnamo 2013.

Huku Man-United wakiwaendea Leicester katika mechi ya mwisho ligini ugani King Power mnamo Julai 26, West Ham watakuwa wenyeji wa Aston Villa ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 17 kwa alama 34 sawa na Watford.