Michezo

Man U waitishiwa Sh11b kutwaa huduma za Jack Grealish

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KLABU ya Aston Villa sasa imewataka Manchester United iwape Sh11 bilioni kwa minajili ya huduma za nahodha wao, Jack Grealish, 24.

Hiki ni kiasi cha fedha ambazo ziliwekwa mezani na Man-United mwanzoni mwa msimu huu kwa minajili ya kumshawishi beki Harry Maguire kubanduka kambini mwa Leicester City.

Ingawa ni matamanio ya Villa kusalia na Grealish uwanjani Villa Park, Nassef Sawaris na Wes Edens ambao ni wamiliki wa kikosi hicho wamekiri kwamba huenda ikawa vigumu kwa kiungo huyo kukataa ofa Man-United.

Kubwa zaidi ambalo huenda likamchochea Grealish kuagana na Villa ni iwapo waajiri wake hao watashindwa kutamba katika michuano tisa iliyosalia katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu na hivyo kuteremshwa ngazi hadi Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship).

Kuondoka kwa Grealish uwanjani Villa Park kutakuwa pigo kubwa kwa Villa ambao walitumia sehemu kubwa ya raslimali zao muhula jana kujisuka upya baada ya kurejea kushiriki EPL.

Iwapo watashushwa daraja, basi Villa watakuwa wepesi wa kukatiza uhusiano na wengi wa masogora wao wa haiba licha ya kwamba wamiliki wao wanajivunia ukwasi wa kima cha Sh170 bilioni.

Mbali na Grealish, Man-United wanahemea pia maarifa ya Isco kutoka Real Madrid, Jadon Sancho wa Borussia Dortmund, James Maddison wa Leicester na chipukizi wa Villa, Carney Chukwuemeka, 16.

Ingawa hivyo, kocha Ole Gunnar Solskjaer ameshikilia kwamba kuja kwa nyota hawa uwanjani Old Trafford kutategemea hatima ya kiungo Paul Pogba ambaye bei yake imepunguzwa sasa kutoka Sh25 bilioni hadi Sh21 bilioni.