Man U washindwa kupiga Chelsea

Man U washindwa kupiga Chelsea

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amesema kwamba baadhi ya maamuzi ya marefa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani yanachochewa na “nguvu za nje”.

Hii ni baada ya masogora wake kulazimishiwa sare tasa na Chelsea katika mchuano ambao mkufunzi huyo raia wa Norway alisisitiza kwamba walinyimwa mkwaju wa penalti.

Refa Stuart Attwell aliyerejelea VAR kwa kipindi kirefu katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo ugani Stamford Bridge, alidumisha maamuzi ya kutowapa Man-United penalti licha ya fowadi chipukizi Callum Hudson-Odoi kuonekana kunawa mpira ndani ya kijisanduku cha Chelsea.

“Ilikuwa penalti ya wazi. Yasikitisha kwamba kwa sasa hatuna kelele za mashabiki wa kulalamikia baadhi ya maamuzi ya utata yanayofanywa na marefa uwanjani,” akasema Solskjaer.

Matokeo ya Man-United katika mchuano huo yaliwapoteza fursa ya kuendelea kufukuzana na viongozi Manchester City kileleni mwa jedwali la EPL msimu huu. Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City waliowapepeta West Ham 2-1 mnamo Februari 27, sasa wanaselelea kileleni kwa alama 62 huku pengo la pointi 12 likitamalaki kati yao na nambari mbili Man-United.

Kwa upande wao, Chelsea kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 44, moja pekee mbele ya mabingwa watetezi Liverpool. Ni pengo la alama moja ndilo linatamalaki kati ya masogora hao wa kocha Thomas Tuchel na West Ham United wanaofunga orodha ya nne-bora jedwalini.

Chelsea walishuka dimbani kwa ajili ya gozi hilo wakilenga kupunguza pengo la alama kati yao na Man-United na kuweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora.

Chini ya Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Lampard baada ya kufutwa kazi na PSG, Chelsea sasa wameshinda mechi sita na kuambulia sare mara tatu pekee kutokana na michuano tisa iliyopita.

Chelsea walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakilenga kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 katika gozi la awali la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) lililowakutanisha na Atletico Madrid ya Uhispania katika mkondo wa kwanza wa kipute hicho mnamo Februari 23 jijini Bucharest, Romania. Ushindi huo uliwaweka pazuri kufuzu kwa robo-fainali za soka ya UEFA msimu huu.

Kabla ya kurudiana na Atletico mnamo Machi 17 nchini Uingereza, Chelsea watakuwa wamepepetana na Man Liverpool, Everton na Leeds United katika EPL, mechi zitakazokuwa kipimo kamili cha uwezo wa kukamilisha kampeni za muhula huu ndani ya nne-bora.

Chelsea hawajawahi kupiga Man-United ligini tangu Novemba 2017, vikosi hivyo viliambulia pia sare tasa katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL uliowakutanisha ugani Old Trafford mwanzoni mwa msimu huu.

Man-United walijitosa ulingoni wakijivunia motisha ya kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Europa League baada ya kubandua Real Sociedad ya Uhispania kwa jumla ya mabao 4-0. Masogora hao wa Solskjaer walifunga magoli hayo katika mkondo wa kwanza kabla ya kulazimishiwa sare tasa katika marudiano ya Alhamisi iliyopita jijini Turin, Italia.

Ufanisi wao huo wa Red Devils uliwapa tiketi ya kuvaana na mabingwa mara saba wa UEFA, AC Milan kutoka Italia katika hatua ya 16-bora ya Europa League kati ya Machi 11-18, 2021.

Man-United ambao ni mabingwa mara 20 wa EPL, sasa watachuana na Crystal Palace na Man-City ligini kabla ya kuwaalika AC Milan kwa mkondo wa kwanza wa Europa League ugani Old Trafford.

Zaidi ya kufukuzia mataji ya EPL na Europa League, Man-United pia wangali katika kipute cha kuwania Kombe la FA na wamepangwa kuchuana na Leicester kwenye robo-fainali mnamo Machi 21, 2021 ugani King Power.

MATOKEO YA YA EPL (Februari 28):

Crystal Palace 0-0 Fulham

Leicester City 1-3 Arsenal

Tottenham 4-0 Burnley

Chelsea 0-0 Man-United

Sheffield Utd 0-2 Liverpool

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Walimu sasa walia, wataka nyongeza mpya ya mshahara

JAMAL MUSIALA: Usimuone alivyo kinda, ana thamani ya Sh3.2...