Michezo

Man U yanyakua afisa mkuu mtendaji wa Man City ili ‘kuwaibia’ siri za ufanisi

January 26th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

MASHABIKI wa Manchester United wamefurahia mageuzi yanayofanyika Old Trafford baada ya Bwanyenye Sir Jim Ratcliffe kununua asilimia 25 ya hisa ya klabu hiyo.

Hii ni baada ya United kuthibitisha kunyakua huduma za Omar Berrada kuwa Afisa Mkuu Mtendaji kutoka Manchester City.

“Klabu hii inajizatiti kuweka kandanda na matokeo katika kila kitu ambacho tunafanya. Kuteuliwa kwa Omar kunawakilisha hatua ya kwanza ya safari hii,” ilisema taarifa ya The Red Devils mnamo Januari 21, 2024.

Mabingwa mara 20 wa Uingereza wamenasa tajiriba iliyoshiba kutoka kwa afisa mkuu wa Manchester City (klabu bingwa duniani na barani Ulaya kwa sasa) na aliwahi kuwa na majukumu makubwa katika usimamizi wa miamba wa Uhispania, Barcelona.

Manchester City ilithibitisha kujiuzulu kwa Omar siku ambayo United iliponyoka na huduma zake.

“Klabu hii inaelewa uamuzi wake wa kutafuta changamoto mpya na tunamtakia kheri,” Manchester City ilisema.

Lakini yaonekana Kocha wa The Cityzens, Pep Guardiola, ametania akisema uteuzi huo hauwezi kubadili chochote Old Trafford.

“Ujuzi wake unaenda kwa United, ndiyo hali halisi,” Pep alisema.

“Lakini Kevin De Bruyne, Erling Haaland wangali Man City. Pengine United wanadhani wakiwa na mtu huyu kila kitu kitabadilika – hongera. Sidhani kama kitafanyika.”