Michezo

Man United itahangaisha wapinzani msimu ujao – Lingard

May 15th, 2019 1 min read

MASHIRIKA NA CECIL ODONGO
 
BAADA ya msimu mbaya, kiungo wa Manchester United Jesse Lingard amesisitiza kwamba timu hiyo itaamka na kupambana vilivyo na wapinzani msimu ujao wa 2019/20.
 
United walishinda mechi mbili tu kati ya nyingine 12 Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) ikielekea ukingoni kilele chake ikiwa kufungwa 2-0 na Cardiff City siku ya mwisho ya ligi.
 
Kufanya huko vibaya kumesababisha Manchester United kuratibishwa kushiriki Ligi ya Uropa baada ya kumaliza katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL tena bila kushinda taji lolote.
 
Hata hivyo, kocha Ole Gunnar Solskjaer atakuwa na wakati mgumu pale dirisha la usajili litakapofunguliwa huku akitarajiwa kuamua wachezaji wa kutemwa, wa kununuliwa na wale watakaosalia.
 
Kwenye mahojiano na Televisheni ya Manchester United (MUTV), Lingard aliahidi kwamba Man U msimu ujao itakuwa moto wa kuotea mbali na akataadharisha timu nyingine dhidi ya kuidharau.
 
“Umekuwa msimu mrefu ambao tuliwajibikia mechi nyingi na tutahitaji kila moja timuni msimu ujao. Lazima tujiandae vizuri wakati wa mazoezi ya kabla ya msimu hasa ikizingatiwa kwamba kocha wetu amekwisha pokezwa kazi ya kudumu ya ukufunzi na klabu.
 
“Tukitia bidii na kurejelea fomu yetu ya awali, basi nina hakika kwamba tutatoa upinzani mkali kwa Manchester City, Liverpool na nyingine zilizomaliza mbele yetu ligini,” akasema Lingard.