Michezo

Man United itang'aa bila Pogba – Gary Neville

September 14th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MLINZI wa zamani wa Manchester United Gary Neville amesema kwamba klabu hiyo baado itang’aa  hata mchezaji nyota na mshindi wa Kombe la Dunia, Paul Pogba akigura uwanja wa Old Trafford. 

Akisisitiza kwamba hakuna mchezaji ambaye ni kubwa kuliko timu, staa huyo wa zamani amemtaka Pogba aliye na umri wa miaka 25 kuheshimu wachezaji wenzake na kocha Jose Mourinho au ahamie klabu nyingine akihisi kwamba hathaminiwi tena Old Trafford.

“Yeye ni mchezaji aliyejaaliwa talanta lakini nitafurahia sana akidhihirisha uongozi timuni kama nahodha. Kama shabiki najua kwamba hakuna mtu mkubwa kuliko timu kwa hivyo ikiwa roho ya Paul ipo kwingine ningemshauri aende kwa sababu timu itaendelea kufanya vizuri hata akikosekana,” akasema Neville akizungumza na jarida la The Times.

Hatima ya Pogba ugani Old Trafford imekuwa hati hati kutokana na madai kwamba uhusiano kati yake na kocha Jose Mourinho umeingia baridi na unaendelea kuzorota.

Katika kikao na wanahabari mwezi Agosti, Mfaransa huyo alifichua kwamba kuna mambo yanayoathiri timu ambayo hawezi kuzungumzia wazi.

Vile vile amekataa kukanusha ripoti za uhamisho zinazoendelea kumhusisha na mabingwa wa Laliga Barcelona ambao wameripotiwa kuwa miongoni mwa klabu mahiri  zilizo katika mstari wa mbele kuwania huduma zake.

Manchester United wanakalia nafasi ya 10 katika msimamo wa jedwali la EPL na watashuka dimbani Septemba 16 kuvaana na Watford ugenini.