Man-United na Chelsea zatoka sare uwanjani Stamford Bridge

Man-United na Chelsea zatoka sare uwanjani Stamford Bridge

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walijiandaa kwa ujio wa kocha mshikilizi Ralf Rangnick kwa kuwalazimishia Chelsea sare ya 1-1 katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Stamford Bridge.

Chini ya Michael Carrick ambaye sasa anatarajiwa kumpisha Rangnick, Man-United waliomweka Cristiano Ronaldo benchi katika kipindi cha kwanza, walifunga bao kupitia Jadon Sancho aliyechuma nafuu kutokana na masihara ya Jorginho katika dakika ya 50.

Chelsea waliomiliki asilimia kubwa ya mpira walipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao katika vipindi vyote viwili vya mchezo na walisawazishiwa na Jorginho kupitia penalti baada ya Aaron Wan-Bissaka kumchezea Thiago Silva visivyo katika dakika ya 69.

Sare hiyo ilikuwa kitulizo kikubwa kwa mashabiki wa Man-United walioshuhudia kikosi chao kikipepetwa na Leicester City, Liverpool, Manchester City na Watford katika mechi za awali ligini chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer aliyepigwa kalamu.

Katika mchuano huo wa kwanza wa EPL kwa Carrick, kiungo huyo wa zamani wa Man-United aliwajibisha Fred, Scott McTominay na Nemanja Matic katika safu ya kati na mbinu hiyo ikachangia kudhibiti makali ya Chelsea. Ronaldo aliletwa uwanjani katika dakika ya 64 japo mchango wake haukuhisika pakubwa.

Katika mechi yake ya kwanza tangu aaminiwe kushikilia mikoba ambayo Man-United walipokonya Solskjaer, Carrick aliongoza mabingwa hao mara 20 wa EPL kucharaza Villarreal ya Uhispania 2-0 katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugenini mnamo Novemba 23, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AS Roma ya kocha Jose Mourinho yashinda mechi tatu...

Vyakula vilivyo na madini ya kalsiamu na umuhimu wake...

T L