Michezo

Man-United na Man-City nguvu sawa katika EPL

December 13th, 2020 3 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer amesema kwamba timu yake ya Manchester United iliridhisha zaidi katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililowakutanisha na Manchester City mnamo Disemba 12, 2020 uwanjani Old Trafford.

Katika mchuano ambao ulikosa matukio ya kusisimua zaidi, vikosi vyote viwili vilicheza kwa tahadhari kubwa bila ya kushambuliana, mbwembwe na mihemko jinsi ilivyo kawaida na upekee wa mechi za sampuli hizo kwenye uwanja wa Old Trafford almaarufu Theatre of Dreams.

Gabriel Jesus na Riyad Mahrez walimwajibisha kipa David De Gea mara mbili pekee katika kipindi cha kwanza huku jaribio la pekee lililofanywa na Man-United langoni mwa wageni wao likiwa kombora lililovurumishwa na Scott McTominay mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na beki Victor Lindelof.

Man-United walijibwaga uwanjani wakitarajiwa kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakiwacharaza Man-City mara tatu kutokana na mechi nne za msimu uliopita wa 2019-20. Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United waliwapiga Man-City katika mechi zote za mikondo miwili ya EPL msimu uliopita.

“Tulimiliki asilimia kubwa ya mpira na kuwazidi maarifa katika idara zote. Nadhani tungewafunga mabao manne kuanzia dakika ya 10 hadi 25,” akatanguliza Solskjaer.

Man-United walidhani walikuwa wamepata penalti katika kipindi cha pili baada ya Kyle Walker kumwangusha Marcus Rashford katika eneo la hatari. Hata hivyo, maamuzi ya refa yalibatilishwa na teknolojia ya VAR iliyobainisha kwamba Rashford alikuwa ameotea wakati akikabiliwa na Walker.

Matokeo hayo yaliwasaza Man-United katika nafasi ya nane jedwalini kwa alama 20, moja pekee mbele ya Man-City.

Man-United walitarajiwa kutumia mchuano huo kuwa jukwaa la kujinyanyua baada ya kichapo cha 3-2 kutoka kwa RB Leipzig mnamo Disemba 8, 2020 kuwabandua kwenye hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Paul Pogba alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Man-United kwenye mchuano huo ila ushawishi wake haukuhisika kabisa uwanjani huku vikosi vyote vikicheza kwa kuogopana.

“Kimkakati, walionekana tishio katika dakika za mwanzo wa kipindi cha kwanza. Walitushambulia kwa mipira ya kushtukiza, nasi tukawa thabiti kabisa katika safu ya ulinzi. Sote tuliridhishwa na sare hiyo,” akaongeza Solskjaer aliyekosolewa pakubwa na mashabiki kwa kutomchezesha sajili mpya Donny van de Beek aliyesajiliwa kutoka Ajax ya Uholanzi kwa Sh5.6 bilioni mwishoni mwa msimu uliooita wa 2019-20.

Man-City waliendeleza rekodi nzuri ya kutofungwa bao katika mechi ya sita mfululizo tangu chombo chao kizamishwe na Tottenham Hotspur kwa kichapo cha 2-0 mnamo Novemba 2020. Beki John Stones wa Man-City aliridhisha zaidi mbele ya kocha wake wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Southgate aliyehudhuria mchuano huo.

Stones, 26, alikuwa sehemu ya muhimu katika fainali za Kombe la Dunia zilizoshuhudia Uingereza wakidenguliwa kwenye nusu-fainali mnamo 2018 nchini Urusi. Hata hivyo, fomu yake iliyoshuka pakubwa tangu mwanzoni mwa msimu uliopita ilionekana kurejea baada ya kuwadhibiti vilivyo wavamizi wa Man-United.

Ili kudhihirisha ukubwa wa kiwango cha ufufuo wa makali ya beki huyo, kocha Pep Guardiola alihiari kumteua Stones kuunga kikosi chake cha kwanza badala ya Aymeric Laporte. Huenda Southgate akapania sasa kumtegemea Stones katika michuano kadhaa ijayo ya kimataifa baada ya Joe Gomez wa Liverpool kupata jeraha.

Man-United kwa sasa hawajapoteza mchuano wowote dhidi ya Man-City katika mechi tatu zilizopita kwenye mashindano yote ambapo wameshinda mara mbili na kuambulia sare mara moja. Hii ni rekodi nzuri zaidi inayojivuniwa na Man-United dhidi ya Man-City tangu Machi 2016.

Man-United hawajafungwa pia na Man-City kwa mara ya kwanza katika mechi tatu zilizopita tangu Oktoba 1995.

Mechi ya Disemba 12 ilikuwa ya tano kushuhudia vikosi hivyo vikiambulia sare kutokana na michuano 47 iliyopita ya EPL. Sare tatu kati ya hizo zimetokana na michuano 11 iliyopita.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuwaendea Sheffield United mnamo Disemba 17 uwanjani Bramall Lane kabla ya kuwaalika Leeds United uwanjani Old Trafford mnamo Disemba 20. Kwa upande wao, Man-City watakuwa wenyeji wa West Bromwich Albion mnamo Disemba 15 kabla ya kuchuana na Southampton uwanjani St Mary’s mnamo Disemba 14, 2020.