Michezo

Man-United pua na mdomo kumsajili beki Alex Telles

September 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA 

MANCHESTER United wameafikiana beki matata wa FC Porto ya Ureno, Alex Telles kuhusu uwezekano wa kumsajili kwa mkataba wa miaka mitano.

Telles amekuwa akiwaniwa na kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa kipindi kirefu ili ashirikiane vilivyo na Luke Shaw na Brandon Williams kwenye safu ya ulinzi.

Ka mujibu wa gazeti la RMC Sport nchini Brazil, Telles amehiari kujiunga na Man-United baada ya kutupilia mbali ofa za Chelsea waliomsajili tayari beki Ben Chilwell kutoka Leicester City.

Telles anatazamiwa kuwa sajili wa pili wa Man-United ambao hadi kufikia sasa wamejinasia huduma za kiungo mvamizi Donny van de Beek kutoka Ajax nchini Uholanzi.

Hadi alipoamua kutua uwanjani Old Trafford, Telles, 27, alikuwa akihemewa pia na miamba wa soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG).

Mkataba kati ya Telles na Porto unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa Juni 2021. Hicho ndicho kiini cha Porto kusisitiza kwamba bei ya nyota huyo ni Sh3.8 bilioni.

Telles aliwajibishwa kwa mara ya kwanza na timu ya taifa ya Brazil mnamo 2019 baada ya kuridhisha vinara wa mabingwa hao mara tano wa Kombe la Dunia akivalia jezi za Porto.

Hadi kufikia sasa, Telles amechezea Porto zaidi ya mechi 150 na akawafungia jumla ya mabao 24 katika mashindano yote.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO