Michezo

Man-United sasa kusajili Bale na Grealish baada ya kutamaushwa na bei ya Sancho

September 13th, 2020 3 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wako radhi kujiondoa katika vita vya kumsajili chipukizi Jadon Sancho wa Borussia Dortmund na badala yake kujinasia huduma za fowadi Gareth Bale kutoka Real Madrid na Jack Grealish ambaye ni nahodha wa Aston Villa.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer amesema kwamba waajiri wake Man-United wametamausha na bei kubwa ya Sh15 bilioni ambayo Dortmund wamesisitiza kwamba ni lazima kwa mnunuzi wa Sancho kuweka mezani ndipo wajinasie maarifa ya fowadi huyo raia wa Uingereza.

“Niliamini kwamba Sancho anegutusaidia kupunguza pengo la alama ambalo Liverpool na Manchester City wametuacha nalo katika kipindi cha misimu miwili iliyopita,” akatanguliza Solskjaer.

“Lakini bei ya Dortmund imetutisha na hawako tayari kulegeza kamba. Naye Sancho anadai mshahara wa Sh84 milioni kwa wiki. Huu ni msimamo ambao kinara wetu Ed Woodward amesema unatamausha,” akaendelea Solskjaer kwa kufichua kwamba sasa wameelekeza mawazo kwa Bale na Grealish ambaye ni nahodha wa Villa.

Real ambao hawajachezesha Bale sana katika mechi yoyote mwaka huu, wako radhi kumtupa kiungo huyo mnadani kwa kima cha Sh3 bilioni.

Man-United ambao tayari wamemsajili Donny van de Beek kutoka Ajax kwa Sh5.6 bilioni, wanatarajia kurasimisha uhamisho wa Bale na Grealish kufikia siku ya mwisho ya usajili mnamo Oktoba 5, 2020.

Rais wa zamani wa Real, Ramon Calderon amesema nyota Gareth Bale “anapoteza muda wake” uwanjani Santiago Bernabeu na ipi haja kwa fowadi huyo mzawa wa Wale na waajiri wake “kupata suluhu ya kudumu” kwa tatizo lililopo haraka iwezekanavyo.

“Inasikitisha sana kuona mchezaji wa haiba ya Bale akisalia kuoza banchi. Naamini kwamba uwezo wa Bale uwanjani badi ni wa kiwango kikubwa kikubwa cha kuhisika na unatosha kumpa nafasi ya kuvalia jezi za kikosi chochote duniani,” akatanguliza Calderon.

“Italazimu Real kuzungumza na Bale na kukomesha masaibu na mahangaiko anayoyapitia mwanasoka huyo. Iwapo Bale hataki kupunguziwa mshahara wake, jambo ambalo linaeleweka, basi itabidi mwafaka kwa mgororo uliopo kutafutwa kwa lazima,” akasema kinara huyo.

Bale, 31, angali na miaka miwili kwenye mkataba wake na Real ambao kwa sasa humpokeza mshahara wa hadi Sh85 milioni kwa wiki.

Katika msimu mzima wa 2019-20, Bale alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Real mara 14 pekee katika mapambano yote na akachezeshwa mara mbili pekee tangu kurejelewa kwa soka ya Uhispania mnamo Juni baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na janga la corona.

Kwa mujibu wa Jonathan Barnett ambaye ni wakala wa Bale, mteja wake alikataa kusafiri jijini Manchester kwa gozi la marudiano ya UEFA ambalo Man-City walishinda 2-1 ugani Etihad kwa sasa alifahamu fika kwamba asingekuwa sehemu ya kikosi cha kwanza wala hangewajibishwa katika katika mechi hiyo.

Mwishoni mwa Julai 2020, Barnett alisisitiza kwamba “Bale haendi popote na atastaafu soka akiwa mwanasoka wa Real hata kama hatawahi kuchezeshwa na Zidane”.

“Kocha Zidane hamtegemei Bale kabisa na sidhani atawahi kuwa sehemu ya mawazo au mipango yake ya baadaye,” akasema Calderon ambaye aliwahi kuongoza usajili wa Cristiano Ronaldo katika kipindi cha miaka mitatu cha urais wake kambini mwa Real.

“Iwapo Zidane atasalia Real, jambo ambalo nina hakika nalo, basi itamlazimu Bale kutafuta njia ya kuondoka Bernabeu kwa sababu Zidane aliyafikia maazimio yake ya kutwaa ubingwa wa La Liga msimu huu bila ya kumhitaji sana Bale,” akasema Calderon.

Mbali na kupendekezea Real kumtoa Bale kwa mkopo huku wakilipia sehemu ya mshahara wake, Calderon amewataka Real kumtia sogora huyo mnadani ili kikosi chochote kinachomhitaji kimsajili bila ada yoyote.

Bale amekuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea Tottenham Hotspur au kuingia katika sajili rasmi ya Newcastle United baada ya uhusiano wake na Zidane kuvurugika.

Fowadi huyo aliondoka Tottenham Hotspur mnamo Septemba 2013 kwa kima cha Sh11 bilioni na amewashindia Real mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), mawili ya La Liga, moja la Copa del Rey, matatu ya Kombe la Dunia miongoni mwa klabu, matatu ya Uefa Super Cup na moja la Spanish Super Cup.

Alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Jiangsu Suning ya China mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki. Hata hivyo, Real walizuia uhamisho wake katika dakika za mwisho kwa sababu walitaka Suning walipie ada yote ya kumsajili.

Inter Miami ya kocha David Beckham nchini Amerika pia iko tayari kuweka mezani Sh7 bilioni kwa minajili ya huduma za Bale.