Man-United wakabwa koo na Southampton ligini

Man-United wakabwa koo na Southampton ligini

Na MASHIRIKA

MAKALI yaliyoshuhudia Manchester United wakipepeta Leeds United 5-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu yalizimwa na Southampton waliowalazimishia sare ya 1-1 uwanjani St Mary’s katika mchuano wa pili mnamo Jumapili.

Chini ya kocha Ralph Hasenhuttl, Southampton walishuka dimbani kwa ajili ya kipute hicho wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Everton katika gozi la awali la ufunguzi wa muhula.

Kikosi hicho kiliwekwa kifua mbele na Fred aliyejifunga kwa upande wa Man-United katika dakika ya 30 baada kuzidiwa maarifa na Che Adams aliyemwajibisha vilivyo kipa David de Gea katika vipindi vyote viwili vya mchezo. Man-United walisawazishiwa na Mason Greenwood katika dakika ya 55.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Man-United alitumia mchuano huo kama jukwaa la kumchezesha kwa mara ya kwanza sajili mpya Jadon Sancho aliyejaza nafasi ya Anthony Martial aliyekosa kuridhisha katika kipindi cha kwanza.

Sare dhidi ya The Saints iliwasaza Man-United wakiwa na alama nne sawa na Everton na Brentford. Ni pengo la pointi mbili ndilo linatamalaki kati ya Man-United na Tottenham Hotspur, Brighton, Liverpool na viongozi wa jedwali Chelsea.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wadau walia sheria za Covid zawafinya

WARUI: Serikali iharakishe maandalizi ya sekondari kwa CBC