Man-United wamfuta kazi kocha Ole Gunnar Solskjaer

Man-United wamfuta kazi kocha Ole Gunnar Solskjaer

Na MASHIRIKA

MECHI ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyokutanisha Manchester United na Watford ugani Vicarage Road mnamo Jumamosi ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer kusimamia kambini mwa The Red Devils.

Vinara wa Man-United waliandaa kikao cha dharura na kufikia maamuzi ya kumtimua Solskjaer chini ya kipindi cha saa 48 baada ya mabingwa hao mara 20 wa EPL kudhalilishwa kwa kichapo cha mabao 4-1 katika pambano hilo.

Wanasoka wa Man-United waliondoka ugani wakiinamisha vichwa kwa aibu huku mashabiki wa kikosi hicho wakizomea Solskjaer pamoja na wasaidizi wake walioonekana wakiomba msamaha wakitoa ‘kwaheri’ zao.

Kwa mujibu wa ripoti, kupigwa kalamu kwa Solskjaer kutagharimu Man-United kima cha Sh1.7 bilioni ikizingatiwa kwamba mkufunzi huyo raia wa Norway alitia saini mkataba mpya wa kuhudumu ugani Old Trafford kwa miaka mitatu zaidi mnamo Julai.

Solskjaer anafurushwa na Man-United yapata miaka mitatu baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa mikoba ambayo miamba hao walimpokonya mkufunzi raia wa Ureno, Jose Mourinho ambaye sasa ananoa AS Roma ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Brendan Rodgers wa Leicester City, Erik ten Hag wa Ajax, Mauricio Pochettino wa Paris Saint-Germain (PSG) na kocha wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane ni miongoni mwa wakufunzi wanaohusishwa na uwezekano mkubwa wa kujaza pengo la Solskjaer ugani Old Trafford.

Hata hivyo, juhudi za Man-United kujinasia maarifa ya Zidane huenda zikazaa nunge ikizingatiwa kwamba mke wa mkufunzi huyo raia wa Ufaransa, Veronique Fernandez, amepiga breki mipango yoyote ya mumewe kuhamia jijini Manchester, Uingereza.

Licha ya kujivunia kikosi thabiti kilichosukwa upya mwanzoni mwa muhula huu baada ya kusajiliwa kwa nyota Cristiano Ronaldo, Raphael Varane na Jadon Sancho, Man-United wameshinda mechi nne pekee kutokana na 13 na wameshinda mechi moja kutokana na saba zilizopita ligini.

Wamejizolea alama 17 baada ya kushinda michuano mitano, kutoka sare mara mbili na kupoteza mechi tano kati ya 12 zilizopita katika EPL. Huku pengo la pointi 12 likitamalaki kati yao na Chelsea wanaoselelea kileleni mwa jedwali, ni alama nne pekee zinazotenganisha Man-United na nambari 16 Watford wanaojivunia idadi sawa ya alama na Aston Villa na limbukeni Brentford.

Mkurugenzi wa masuala ya kiufundi kambini mwa Man-United, Darren Fletcher, ndiye anatarajiwa kuongoza kikosi cha Red Devils kitakachoelekea Uhispania hapo kesho kuvaana na Villarreal ya kocha Unai Emery katika mkondo wa pili wa gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Fletcher atasaidiwa kazi na Michael Carrick ambaye atasalia ugani Old Trafford licha ya kuwa sehemu ya benchi ya kiufundi iliyoongozwa na Solskjaer kushindia Man-United mechi mbili pekee kati ya nane zilizopita.

Baada ya kukwaruzana na Villarreal ambao nusura wawazamishe katika mkondo wa kwanza, Man-United watarejelea kampeni za EPL kwa vibarua vigumu dhidi ya Chelsea, Arsenal na Crystal Palace kwa usanjari huo.

Ingawa kitumbua cha Solskjaer kilianza kuingia mchanga mnamo Septemba 22 baada ya Man-United kudenguliwa na West Ham United kwenye Carabao Cup, masaibu yao yalizidishwa na vichapo kutoka kwa Leicester (4-2), Liverpool (5-0) na Manchester City (2-0).

Watford waliwateremkia Man-United kwa wepesi zaidi mnamo Jumamosi baada ya beki na nahodha Harry Maguire kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano na kufurushwa uwanjani katika dakika ya 69. Kipa David de Gea alisema kichapo kutoka kwa Watford kilikuwa cha “kuaibisha” na “jinamizi”.

Solskjaer alishikilia mikoba ya ukufunzi kambini mwa Man-United hadi Disemba 2018 kabla ya kupokezwa mkataba wa kudumu wa miaka mitatu mnamo Machi 2019 kisha kuurefusha hadi 2024 mnamo Julai.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mganda avunja rekodi ya dunia mbio za kilomita 21...

MALEZI KIDIJITALI: Je, kuwapa watoto uhuru ni kuwaharibu?

T L