Michezo

Man United watamani Bissaka na Van Aanholt wa Crystal Palace

May 16th, 2019 2 min read

MASHIRIKA NA GEOFFREY ANENE

Manchester United inapanga kuvamia ngome ya Crystal Palace kutafuta huduma za mabeki Aaron Wan-Bissaka na Patrick Van Aanholt kwa Sh6.4 bilioni.

Kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer ameweka wazi malengo yake ya kutaka kuimarisha safu ya nyuma katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho na amewatupia macho nyota hao wa Palace na kuwaweka juu ya orodha ya wachezaji anataka.

Bissaka, 21, anaongoza orodha hiyo ya wachezaji wanaofanya United kukosa usingizi, huku hamu yao katika Van Aanholt ikatarajiwa kugawanya wapenzi wa soka.

Kwa mujibu wa gazeti la Sun, United iko macho kupata huduma za wachezaji wote wawili katika mpango unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh6.4 bilioni.

Solskjaer majuzi alikuwa amebadilisha mpango wake wa kufanya shughuli ya uhamisho, akielekeza juhudi zake kwa wachezaji walio na umri chini ya miaka 24.

Bissaka anafaa katika mpango huo, huku United pia ikitafuta mrithi wa muda mrefu wa nafasi ya Ashley Young, ambaye pamoja na Diogo Dalot, ndiye beki wa pembeni kulia wa United kufuatia kuondoka kwa Antonio Valencia.

Kocha huyo wa United anaamini kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 ana nafasi kubwa ya kuimarika na yuko tayari kumtia katika timu yake moja kwa moja msimu ujao wa 2019-2020.

Licha ya beki wa pembeni kushoto Luke Shaw kutawazwa mchezaji bora wa United wa msimu 2018-2019, Solskjaer anataka kuongeza mchezaji mzoefu kutoka Ligi Kuu ya Uingereza kutoa ushindani katika nafasi hiyo.

Hiyo ndiyo sababu United inasemekana sasa inawazia kutafuta Van Aanholt. Raia huyu wa Uholanzi alitumiwa sana na Palace msimu uliopita, akisakata mechi 40 na kupachika mabao manne katika mashindano yote.

Hata hivyo, United huenda ikakabiliwa na ushindani mkali kupata sahihi ya Van Aanholt, 28, ambaye amehusishwa na klabu kadhaa katika Ligi Kuu ya Italia.

Licha ya mipango ya Palace kutaka kukwamilia wachezaji wote wawili, United inasalia na matumaini kwamba itakubaliana na klabu hiyo kupata huduma za Bissaka na Van Aanholt.