Man-United wateua kocha Rangnick kushikilia mikoba yao hadi mwisho wa msimu huu wa 2021-22

Man-United wateua kocha Rangnick kushikilia mikoba yao hadi mwisho wa msimu huu wa 2021-22

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamemteua Ralf Rangnick kushikilia mikoba yao kwa muda hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22 hadi watakapomwajiri kocha wa kudumu wa kumrithi mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 63 atashirikiana na Michael Carrick aliyeaminiwa kushikilia mikoba ambayo Solskjaer alipokonywa na Man-United mnamo Novemba 21 kutokana na msururu wa matokeo duni, kilele chake kikiwa kichapo cha 4-1 kutoka kwa Watford ugani Vicarage Road.

Rangnick anatua ugani Old Trafford baada ya kuacha kazi ya kuwa mkuu wa masuala ya makuzi ya soka kambini mwa Lokomotiv Moscow, Urusi.

Mwishoni mwa msimu huu, Rangnick atasalia ugani Old Trafford kwa miaka miwili zaidi ambapo atatarajiwa kutoa ushauri wa mara kwa mara kwa kocha mpya atakayeajiriwa na Man-United.

Mchuano wake wa kwanza kambini mwa Man-United ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ni gozi litakalowakutanisha na Arsenal mnamo Disemba 2, 2021.

Rangnick anajivunia tajriba pana ya ukufunzi na anastahiwa pakubwa na wakufunzi wenzake raia wa Ujerumani – Jurgen Klopp wa Liverpool na Thomas Tuchel wa Chelsea.

Aliwahi kuongoza Ulm kupandishwa ngazi hadi Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya kwanza katika historia kabla ya kupokezwa mikoba ya Stuttgart, Hannover, Hoffenheim, Schalke na RB Leipzig.

Alisaidia Schalke kutwaa taji la German Cup mnamo 2011 na akaongoza RB Leipzig kutinga fainali ya kipute hicho mnamo 2019.

Akidhibiti mikoba ya Schalke mnamo 2010-11, aliongoza kikosi hicho kutinga nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambapo walipepetwa 6-1 na Man-United waliozamishwa na Barcelona kwenye fainali.

Carrick amesimamia michuano miwili iliyopita ya Man-United tangu Solskjaer apigwe kalamu na akaongoza mabingwa hao mara 20 wa EPL kupiga Villarreal 2-0 kwenye UEFA ugenini kisha kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Chelsea ligini ugani Stamford Bridge.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jinsi maafisa, viongozi walihusika katika sakata ya uuzaji...

Serikali yadhamiria kuzima matumizi ya makaa, kuni katika...

T L