Na MASHIRIKA
MARCUS Rashford aliendeleza ubabe wake wa kufunga mabao tangu kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar kwa kucheka na nyavu za Crystal Palace na kusaidia waajiri wake Manchester United kusajili ushindi wa 2-1 ugani Old Trafford mnamo Jumamosi.
Bruno Fernandes alifungulia Man-United karamu ya mabao kupitia penalti kunako dakika ya saba baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba beki Will Hughes alikuwa amenawa mpira.
Ingawa Rashford alifanya mambo kuwa 2-0 baada ya kukamilisha krosi ya Luke Shaw katika dakika ya 62, Palace walirejea mchezoni baada ya kiungo Carlos Casemiro kuonyeshwa kadi nyekundu. Bao la Rashford lilikuwa lake la 11 katika mashindano yote ambayo amechezea Man-United tangu arejee nyumbani kutoka Qatar mnamo Disemba 2022.
Casemiro alidhihirisha utovu wa nidhamu kwa kumkabili visivyo Hughes baada ya Antony kulalamikia kuchezewa kivoloya na Jeffrey Schlupp.
Kuondolewa uwanjani kwa Casemiro kulilemaza safu ya kati ya Man-United na hivyo kuwapa Palace fursa ya kufungiwa na Schlupp baada ya kukita kambi langoni mwa wenyeji wao.
Goli hilo liliwapa Palace motisha zaidi na kumweka kocha Erik ten Hag katika ulazima wa kuleta ugani mabeki Harry Maguire na Victor Lindelof walioshirikiana vilivyo na Lisandro Martinez pamoja na Raphael Varane kuzima makombora ya wavamizi wa Palace.
Ushindi wa Man-United ulikuwa wao wa 13 mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani wa Old Trafford na uliwapaisha hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 42, mbili zaidi kuliko nambari nne Newcastle United waliolazimishiwa sare ya 1-1 na West Ham United uwanjani St James’ Park. Palace kwa sasa wanakamata nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 24 baada ya mechi 21.
Kukosekana kwa Casemiro ambaye sasa atakosa mechi zijazo za EPL dhidi ya Leeds United na Leicester City kutaacha Ten Hag katika ulazima wa kutegemea zaidi maarifa ya Fred na Rashford ambaye sasa anajivunia mabao 19 katika mashindano yote muhula huu wa 2022-23.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO