Michezo

Man United yakalifisha Leeds United 4-0

July 17th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MANCHESTER United FC ilionyesha mchezo wa juu na kuichabanga Leeds United 4-0 kwenye mechi ya kirafiki iliyoandaliwa mjini Perth, Australia Jumatano huku ikiendelea kujifua kwa msimu mpya wa 2019/20.

Mshambulizi Marcus Rashford na Mason Green walifunga mabao mawili kila moja na pia kuongoza vizuri safu ya mbele ya mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu(EPL) kwenye mechi hiyo iliyoshirikisha timu hizo mbili zenye uhasama wa kihistoria wa tangu jadi.

Mlinzi matata Phil Jones aliongeza bao la tatu kisha Antony Martial akafunga ukurasa wa mabao kwa kuchanga kiufundi mkwaju wa penalty uliotunukiwa Man United kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika.

Greenwood aliwaweka The Red Devils kifua mbele kunako dakika ya saba baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Wan-Bissaka ambaye pasi yake ilioana vyema na nyota Paul Pogba anayezidi kuandamwa na tetesi za kuhamia Real Madrid ya Uhispania.

Rashford ambaye kombora lake liligonga mtambapanya mapema baada ya mechi kuanza, naye alifunga bao la pili kunako dakika ya 27 baada ya kumegewa pasi na chipukizi MacTominay.

Makali ya safu ya mbele ya Manchester United yaliyodhihirika kwenye mtanange huo ni habari nzuri kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye yupo kwenye hatari za kupoteza huduma za mshambulizi mahiri raia wa Ubelgiji Romelu Lukaku anayewindwa na vigogo wa Italia AC Milan.

Solskjaer wiki jana alionyesha ishara ya kutowategemea washambulizi wenye majina makubwa, akionekana kupendelea ushirikiano wa Rashford na Martial huku msimu mpya ukijongea mwezi Agosti.

Msimu huo mpya utaanza Agosti 9 huku Manchester United wakitifua vumbi dhidi ya mahasimu wao wa tangu jadi Chelsea kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi.