Michezo

Man-United yasajili mtoto wa mwanasoka Wayne Rooney

December 18th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MTOTO wa mwanasoka Wayne Rooney amepania kufuata nyayo za babaye mzazi kwa kuingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Manchester United.

Kai, 11, alionekana kwenye picha akiwa pamoja na babaye na mamaye mzazi Colleen wakati alipokuwa akitia saini mkataba na kikosi cha Man-United mnamo Alhamisi uwanjani Old Trafford.

Rooney ambaye alichezea Man-United kati ya 2004 na 2017 alisema kwenye mtandao wake wa Instagram: “Ni siku yenye tija na fahari kubwa. Kai sasa ni mchezaji wa Man-United. Jitahidi kabisa mwanangu.”

Katika baadhi ya picha zilizoibua msisimko mkubwa mitandaoni, Kai alionekana akiwa amevalia jezi nambari 10 mgongoni. Nambari hiyo ni sawa na iliyokuwa kwenye jezi zilizokuwa zikivaliwa na Rooney katika kiwango cha soka ya klabu na timu ya taifa.

Rooney ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Man-United akijivunia kufungia kikosi hicho jumla ya mabao 253 kutokana na mechi 559 katika kipindi cha miaka 13.