Michezo

Man-United yatiwa katika zizi gumu UEFA

October 3rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wametiwa katika zizi moja na Paris Saint-Germain (PSG), RB Leipzig na Istanbul Basaksehir kwenye hatua ya makundi ya kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool, watavaana na Ajax ya Uholanzi, Atalanta ya Italia na Midtjylland ya Denmark katika Kundi D.

Chelsea watapepetama na mabingwa wa Europa League Sevilla, Krasnodar na Rennes ya Ufaransa katika Kundi E.

Manchester City wametiwa katika Kundi D kwa pamoja na FC Porto, Olympiakos na Olympique Marseille ya Ufaransa.

Kwingineko, nyota Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wataonana uso kwa macho kwa mara nyingine uwanjani baada ya Juventus anayochezea Ronaldo kupangwa na Barcelona ya Messi katika Kundi G linalowajumuisha pia Dynamo Kyiv na Ferencvaros.

Mabingwa watetezi wa UEFA, Bayern Munich kutoka Ujerumani watavaana na Atletico Madrid ya Uhispania katika Kundi A ambalo pia linawajumuisha Salzburg na Lokomotiv Moscow.

Droo hiyo iliyoshuhudia Real Madrid wakipangwa katika Kundi B pamoja na Inter Milan, Shakhtar Donetsk na Borussia Monchengladbach, ilifanywa Oktoba 1, 2020 bila kuwepo kwa maafisa wa klabu mbalimbali kwa sababu ya janga la corona.

Mechi za hatua ya makundi katika UEFA msimu huu zitaanza kusakatwa Jumanne ya Oktoba 20, 2020 huku fainali ikitazamiwa kusakatiwa mnamo Mei 29, 2021 uwanjani Ataturk, jijini Istanbul, Uturuki.

DROO YA UEFA 2020-21:

KUNDI A: Bayern Munich, Atletico Madrid, Salzburg, Lokomotiv Moscow

KUNDI B: Real Madrid, Shakhtar Donetsk, Inter Milan, Borussia Monchengladbach

KUNDI C: Porto, Manchester City, Olympiakos, Marseille

KUNDI D: Liverpool, Ajax, Atalanta, Midtjylland

KUNDI E: Sevilla, Chelsea, FK Krasnodar, Rennes

KUNDI F: Zenit St Petersburg, Borussia Dortmund, Lazio, Bruges

KUNDI G: Juventus, Barcelona, Dynamo Kyiv, Ferencvaros

KUNDI H: Paris St-Germain, Manchester United, RB Leipzig, Istanbul Basaksehir

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO