Habari za Kitaifa

Manaibu gavana walia majukumu yao kupewa wake wa magavana


NAIBU gavana alisimulia wabunge mateso wanayovumilia chini ya wakubwa wao kwa kukosa majukumu maalum katika serikali ya kaunti, ikiwemo majukumu yao kukabidhiwa wake wa magavana.

Naibu Gavana wa Nandi Yulita Mitei alisema mara nyingi baadhi yao hawaarifiwi kuhusu mikutano ya serikali ya kaunti ili kuhakikisha kwamba wamezimwa kabisa.

Kama sehemu ya kudhalilishwa, alisema, majukumu ambayo wanapaswa kufanya yanakabidhiwa wake wa magavana wa kaunti, makarani wa kaunti au mawaziri wa kaunti na kuwafanya tu watazamaji.

Katika visa vingine, wengine hunyimwa magari rasmi huku wale wanaobahatika kuwa na magari wakinyimwa mafuta ya magari hayo.

Bi Mitei alisema kuwa takriban asilimia 90 ya manaibu gavana 47 wana mgao halisi wa bajeti kuendesha afisi zao.

Akiwa mbele ya kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi na Uhusiano wa Kiserikali Jumatano, Agosti 28, 2024 alisema baadhi ya wakuu wa kaunti wanachukulia wadhifa wa naibu gavana kama kiambatisho kisichohitajika ilhali walifanya kampeni pamoja.

Naibu gavana mwingine aliambia kamati inayoongozwa na Seneta wa Wajir Mohamed Abass jinsi wakati mmoja wahuni walitumwa kumvuruga alipojaribu kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri la kaunti bila mwaliko baada ya kutofautiana na bosi wake.

Manaibu gavana walisema kuwa ni watano tu kati yao walio na uhusiano mzuri wa kufanya kazi na wakubwa wao, na wengine huvumilia ilhali waliounda Katiba ya 2010 walitarajia ushirikiano wa kikazi kati ya maafisa hao wawili.

“Wakati wa Uchaguzi Mkuu tunachaguliwa kwa pamoja lakini tunapoingia ofisini hatuwezi tena kufanya kazi pamoja licha ya jukumu tunalotekeleza kuingia ofisini,” alisema Naibu Gavana wa Laikipia Reuben Kamuri, ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano wa manaibu magavana.

“Tunahitaji kuziba pengo katika sheria kuhusu majukumu ya manaibu wa gavana mara moja. Ikiwa afisa hatawezeshwa, tunatarajia vipi atatekeleza majukumu yake” alisema Bi Mitei.

Baadhi ya manaibu gavana walisimulia jinsi wanadhalilishwa, huku baadhi ya magavana wakikabidhi majukumu ambayo wanapaswa kutekeleza kwa wasaidizi wa kibinafsi wa wakubwa wao.

Manaibu magavana 11 sasa wanataka Seneti kushinikiza mabadiliko ya Sheria ya Serikali za Kaunti ili kuwa na majukumu yanayofafanuliwa wazi na mgao wa bajeti na hatimaye kumaliza vita vya kudumu na wakubwa wao.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni pamoja na kumteua afisa mkuu atakayesimamia masuala ya ofisi ya naibu gavana, kuratibu usimamizi, kupanga na kusimamia utekelezaji wa usimamizi na kukabiliana na maafa ndani ya kaunti.

Mengine ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya serikali ya kaunti na kushiriki maazimio katika idara zote za kaunti, kuwa mwenyekiti wa kamati ndogo kuu za kaunti pamoja na kusaidia gavana katika uratibu na usimamizi wa sekta za serikali ya kaunti.

Hii ni pamoja na kufanya kazi nyingine yoyote ambayo wanaweza kuagizwa na gavana.