Manaibu gavana waomba wapewe kazi za kufanya

Manaibu gavana waomba wapewe kazi za kufanya

Na JOSEPH WANGUI

MUUNGANO wa Manaibu Gavana unataka Katiba ifanyiwe mageuzi kusudi majukumu yao yaorodheshwe ili kuhakikisha wanahusishwa kikamilifu katika uendeshaji wa shughuli za kaunti.

Wanataka kipengele kijumuishwe kwenye katiba kitakachowalazimisha magavana kuwatengea wizara mahususi wasimamie.

Pia manaibu hao wa gavana wanataka wapewe mamlaka ya kuwakilisha serikali zao katika mabunge ya kaunti wakati wa vipindi vya maswali na majibu.

“Shinikizo zetu zisifasiriwe kumaanisha kuwa tunapigania mamlaka zaidi. Haja yetu kuu ni kuhakikisha kuwa majukumu ya manaibu gavana yanawekwa wazi ili afisi hii iweze kuwahudumia watu,” akasema mwenyekiti wa muungano huo, Bi Caroline Karugu ambaye ni Naibu Gavana wa Nyeri.

Aliongeza kuwa Afisi ya Naibu Gavana inahitaji ulinzi wa kisheria kwa sababu ni sehemu ya afisi muhimu katika mfumo mzima wa serikali ya ugatuzi.

“Ikiwa jopokazi la mpango wa maridhiano (BBI)litafeli kujumuisha pendekezo letu katika ripoti yake tutawasilisha pendekezo letu kwa wabunge,” akasema Bi Karugu.

Wakati huu, baadhi ya manaibu gavana hunyanyaswa na mabosi wao kwa kutotengewa wasaidizi, magari au kutengewa majukumu maalum kutokana na sababu za kisiasa.

Katiba ya sasa ilifeli kubainisha majukumu mahususi ya manaibu gavana. Kipengele cha 179 (4 na 5) kinasema kuwa Naibu Gavana ni Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa Kaunti na endapo gavana hayuko, anaweza kutekeleza majukumu ya afisi hiyo.

Bi Karugu pia alisema muungano huo unataka utaratibu wa kuondolewa afisini kwa naibu gavana uwekwe kwenye katiba sawa na ulivyo utaratibu wa kuondolewa kwa magavana.

Wataalamu walikuwa wametaja kazi ya naibu gavana ni mojawapo ya afisi salama kwa sababu hamna utaratibu wazi wa kumwondoa mshikilizi wake.

“Hamna kipengeleza waziwazi katika Katiba na Sheria ya Serikali za Kaunti kinachoelezea utaratibu wa kumwondoa afisini naibu gavana. Ni muhimu kuwe na vipengeleza kama hivi katika sheria kwa manufaa ya utawala wa Kaunti. Afisi ya Naibu Gavana ni Kuu na hivyo kunapasa kuwe na utaratibu mahsusi wa kisheria wa kumwondoa mshikilizi wa afisi hizo,” akasema.

Lengo la sheria hiyo, akasema, ni kuhakikisha kuwa utaratibu wa kumwondoa naibu gavana afisini unaongozwa na vigezo vilivyoko kwenye katiba na sheria husika.

Kuhusu namna afisi ya Naibu Gavana inaweza kusalia wazi, manaibu gavana, wanataka kipengele cha 182 (1) (d) kifanyiwe mageuzi.

Kipengele hicho kinasema kuwa afisi hiyo itasalia wazi ikiwa naibu gavana atahukumiwa kwa kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha angalau miezi 12 gerezani.

You can share this post!

KRA kuzindua mfumo mpya wa kodi Nairobi

Shabana FC katika hatari ya kusambaratika

adminleo